Advertisement |
Mhandisi Kapulya Musomba |
NA WILLIAM
SHECHAMBO
SHIRIKA la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC), kama yalivyo mashirika mengine ya umma hapa nchini,
limekiri kuwa na mchango mkubwa kwenye kuifikia Tanzania ya viwanda inayolengwa
na serikali ya awamu ya tano.
Mchango huo
ni kulingana na nafasi yake inayopewa uzito na shughuli zake zilizoko kwa
mujibu wa sheria Sheria ya Mashirika ya Umma Namba
17 ya mwaka 1969 ya sheria za Tanzania ilioondolewa na kubadilishwa na Kifungu
Namba 257 cha Sheria ya Mashirika ya Umma cha mwaka 2002 cha Sheria za
Tanzania.
Kifungu hiko kwa kupitia notisi
ya Serikali Namba 140 ya Mei 30 mwaka 1969, Shirika hili lilianza shughuli
rasmi mwaka 1973 chini ya usimamizi wa msajili wa hazina na baadaye lilikabidhiwa
kwa Wizara ya Nishati na Madini.
Shughuli kuu
za shirika kwa wakati huo zilikuwa ni kusimamia shughuli za kampuni ya Mafuta ya AGIP - Azienda Generale Italiana
Petroli ambayo ni Kampuni ya Mafuta ya Italia.
Shughuli za utafutaji mafuta na
gesi asilia nchini zilianza miaka ya 1950 kupitia Kampuni hiyo ya Agip kutoka
Italia ambapo licha ya shughuli hizo kuanza miaka ya 1950, ilifanya ugunduzi wa
kwanza katika Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi mwaka 1974 ambao ulifuatiwa
na ugunduzi mwingine katika eneo la Mnazi Bay (Mtwara) mwaka 1982.
Hata hivyo, historia inaonesha
kwamba gesi hiyo asilia haikuendelezwa kwa kuwa ilionekana haina manufaa ya kiuchumi kwa nchi wakati huo
kutokana na teknolojia kuwa bado chini.
Baada ya ugunduzi huo, TPDC
iliendelea kufanya utafiti ikiwa ni pamoja na kuchimba visima mbalimbali kwa
ajili ya kuthibitisha kiasi cha gesi asilia kilichopo katika maeneo ambako gesi
asilia iliyogunduliwa.
Ilipofika Novemba mwaka 2014,
kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini kilielezwa kuwa ni futi za ujazo
trilioni 53.28 (53.28TCF), ambazo kwa mujibu wa wataalamu akiwemo aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini kwa wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo, kilikuwa
ni kiasi kikubwa cha kumaliza matatizo ya nishati nchini.
Serikali katika kuhakikisha kuwa inanufaika
na rasilimali ya gesi asilia
iliyogunduliwa, kupitia TPDC ilianza
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mitambo mbalimbali ya kisasa.
Mitambo hiyo ilijumuisha ile ya kusafisha
gesi asilia katika maeneo ya Madimba mkoani Mtwara na kule Songo Songo, Lindi
sambamba na bomba la kusafirisha gesi asilia hiyo kutoka Mtwara, kupitia
Somanga Fungu (Lindi), Pwani mpaka Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa serikali lengo la
kutekeleza miradi hiyo ni kuhakikisha
kuwa gesi asilia mbali na
matumizi mengine, itumike katika
kuzalisha umeme ambao kwa sasa unazalishwa kwa kutumia mafuta ambayo ni ghali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Mhandisi Kapulya Musomba, anathibitisha kufanikiwa kwa lengo hili la
serikali kwamba kwa sasa, kiasi cha fedha zinazotumiwa na serikali kuagiza
mafuta ya mitambo ni asilimia chini ya 1 kutoka gharama za awali zilizokuwa
Dola za Marekani Bilioni 1 kila mwaka.
“Hii ni kutokana na kwamba sasa hivi gesi iliyopo
nchini inatosheleza matumizi ya mitambo iliyohitaji mafuta awali na kwa bahati
nzuri mitambo mingi mikubwa inayoingizwa nchini siku hizi ikiwemo ile ya
TANESCO ina sehemu ya kutumia gesi,” anasema.
Mkurugezi huyo anasema umma unapaswa kufahamu kwamba
TPDC ni kitovu cha Tanzania ya viwanda kwa kuwa viwanda vinahitaji nishati ya
umeme ili vifanye kazi na katika hilo, hadi sasa asilimia 50 ya umeme wa
Shirika la Umeme Tanzania inazalishwa kutokana na gesi asilia.
Anasema tangu kuingia madarakani
kwa serikali ya awamu ya tano, TPDC imeendelea na kasi ya kutekeleza mikakati
yake ikiwa ni pamoja na kushiriki na kujiingiza katika
utafiti, maendeleo, uzalishaji na ugawaji wa mafuta na gesi na huduma
zinazohusiana na hayo.
Pia kuweka mazingira mazuri ya
biashara, kulinda mgawanyo wa taifa wa mazao ya mafuta ghafi na wakati huo huo
kuendeleza ubora na kiwango cha usalama kwa kulinda watu, mali na mazingira.
Si hayo
tu, anaeleza kuwa lengo ni kudhihirisha mtazamo wao kama shirika ambao ni kuongoza kwenye ushindani wa
kitaifa, kimataifa katika hali ya kujali mazingira kwa faida ya wadau wote huku
ikiendelea na kutekeleza wajibu wa shirika kwa taifa, ambao miongozo yake ipo
kisheria.
Kuhusu suala la mchango wa TPDC
na maendeleo ya viwanda hapa nchini, anasema mfano hai ni pale shirika
lilipotangaza kutoa nafasi ya kupokea maombi kwa viwanda kuunganishiwa nishati
ya gesi asilimia.
Anasema kwa kipindi kifupi
walipokea maombi ya viwanda takriban 47 kutoka mkoa wa Dar es Salaam na Pwani
huku Pwani ikiongoza kwa kuwa na maombi mengi ya viwanda takriban 44.
Pia anasema wana mpango wa
kusambaza gesi asilia kwenye mikoa mingine hususan Dodoma na Tanga ambako ili
kufika huko ni lazima mikoa mingine ipate jambo linalofanyiwa utafiti kwa sasa
ili ujenzi wa miundombinu uanze.
Pamoja na hayo anafafanua kuwa
kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kuna eneo la kilomita za eneo zaidi ya 540
ambazo ziko wazi kwa uwekezaji wa viwanda vikubwa na ambalo linafikiwa kwa
ukaribu na bomba kubwa la gesi asilia hivyo fursa za uwekezaji zipo na nishati
ya uhakika.
“Unaweza kuona kuwa kutokana na
kazi inayofanyika siku hizi watanzania wanaanza kusahau matatizo ya umeme kwa
sababu nishati inazaliwa kwa wingi.
“Kwa mfano awali tulizoea umeme
unakatika hata saa saba mpaka 10 kwa siku na watu wanaona sawa tu lakini leo
nusu saa umeme ukikatika ni malalamiko kila kona ya nchi,” anasema.
Mkurugenzi huyo wa TPDC anasema mbali
na viwandani, shirika liko kwenye mpango wa kusambaza gesi asilia kwenye makazi
ya watu kama ilivyoeleza awali, ambapo inafungua milango kwa wawekezaji
washirikiane na TPDC kuwekeza kwenye mradi huo.
“Lengo ni kutunza mazingira kama
inavyofahamika kwamba mkaa unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira
na kwa kiasi kikubwa wananchi wengi wanatumia nishati hii,” anafafanua.
Hata hivyo anasema changamoto
kubwa ni kwamba utaratibu wa kufunga miundombinu ya gesi
asilia si kwa mitungi
bali ni mifumo ya mabomba ambayo kutokana na namna ilivyo kwa ujenzi wa
kitanzania kazi kubwa ya kitaalamu inatakiwa kufanyika ili kufanikisha hilo.
Katika kueleza mipango ya kuuza
gesi nje ya nchi kwa hali ya kimiminika na kuongeza kipato cha taifa anasema
kiwanda kitajengwa mkoani Lindi muda wowote huku mradi wa bomba la mafuta
kutoka Uganda kuja Tanzania ukiwa kwenye hatua ya makadirio ya awali ikiwemo
kuwalipa wananchi.
“Tunaamini ifikapo mwaka 2020,
mafuta ya kwanza kutoka nchini Uganda yataanza kuingia Tanzania kwa sababu
tayari wakuu wetu wa nchi hizi mbili wameshasaini mikataba ya kuruhusu mradi
huu mkubwa kuanza rasmi,” anasema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Bodi ya TPDC, Profesa Sufian Bukurura, anasema nishati ya gesi ina unafuu wa
bei kulinganisha na nishati yoyote ya jamii za mafuta hivyo mchango wa TPDC kwa
maendeleo ya viwanda nchini ni mkubwa.
Anasema TPDC kwenye kuonesha
mchango wake wa moja kwa moja kwenye uchumi wa viwanda unaowekewa msisitizo na
serikali iliyopo madarakani unadhihirika kwa faida wanayoipata wawekezaji wa
viwanda mkoa wa Pwani.
“Mkoa wa Pwani hasa wilaya ya
Mkuranga amabyo ndio ina viwanda vingi vikubwa vilivyokamilika, una bahati
kwamba bomba la gesi limepita hivyo moja ya kiwanda cha mfano ni Goodwill
Ceramic, ambacho ni cha kwanza kuunganishiwa gesi kutoka bomba letu kubwa,”
anasema.
Aidha anasema TPDC ina
ushirikiano mzuri wa wakazi wa vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba kuu la gesi
lakini ni wajibu wa kila mwananchi kwa nafasi yake kutambua kuwa wajibu wa
kutunza miradi ya serikali iliyoigharimu nchi fedha nyingi inatunzwa na kila mtu.
“Unaweza usilipwe fedha lakini
kwa kutoa taarifa unapoona mtu mwingine anahujumu miradi ya gesi, unakuwa
umeokoa kuangamiza taifa lako na kizazi chako kijacho kwa miaka mingi ijayo,”
anafafanua Profesa huyo.
Wananchi wao wanasema
ni dhahiri kuwa TPDC lina mchango mkubwa wa kuitoa kimasomaso Tanzania kwenye
uchumi wa viwanda, kwa sababu bila nishati ya uhakika hakuna viwanda wala treni
za mwendo kasi.
“Wafanye kazi, waepuke mikataba
pori kama ile ya Acacia, wawe macho ili gesi na mafuta vipatikane vikauzwe kwa
bei halali nje ya nchi na hapa nchini zitumike ipasavyo kulishia viwanda
maendeleo tuyaone hata kabla ya 2020,” anasema Felician Kolimba.
Juma Kilowoko anasema viwanda
vyote vikubwa nchini havipaswi kutumia umeme wa maji na badala yake vifungiwe
mifumo ya umeme wa gesi asilia ili ule wa maji uende kwa wananchi pekee.
Anasema kama ilivyofanywa kwenye
mvutano baina ya serikali na kiwanda cha Aliko Dangote, Machi mwaka huu, TPDC chini ya Wizara ya Nishati, viwanda vingine vikubaliane juu ya bei ya mauziano
ya gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya viwanda na kukuza uchumi wa taifa kwa
kuuza bidhaa nje ya nchi.
0 comments: