Saturday, April 14, 2018

FCC yawanoa wadau wa biashara, viwanda

ad300
Advertisement
WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesema wafanyabiashara na wenye viwanda nchini, wanapaswa kufuata utaratibu katika uwasilishaji malalamiko, mapendekezo kuhusu usimamizi wa sheria za biashara badala ya kulalamikia pembeni.



Imesema usimamizi wa sheria zikiwemo zinazohusu usimamizi wa soko, upo kisheria licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa sambamba na faida, lakini msingi wa maendeleo kwenye mataifa yote duniani unaanzia kwenye utekelezaji mzuri wa sheria na usimamizi wa soko.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Aristides Mbwasi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel, kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa biashara nchini kilichoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC).

Akisoma hotuba ya katibu mkuu, Aristides amesema Tume ya Ushindani ni chombo muhimu kilichoanzishwa ili kusimamia utendaji na ufanisi wa mfumo wa soko hapa nchini, hivyo wafanyabiashara ni miongoni mwa wadau wakubwa wa taasisi hiyo.

Hata hivyo, amesema wakati wa utekelezaji wa majukumu yake, inawezekana kukatokea malalamiko kutoka kwa upande wa pili, ambapo ili kupata ufumbuzi hakuna budi pande zote zikaa na kuzungumza kwa utaratibu uliowekwa.

Amesema semina za kuelimishana na kushauriana kama ambayo aliifungua jana, ni njia mojawapo ya kuwakutanisha pande tofauti tofauti na kuzungumza yanayowahusu kwa lengo la kutoka na msimamo mmoja wenye lengo la kujenga.

"Wasilisho lenu kwenye semina hii linaweza kuboresha miundo ya kisera na kisheria kwa kuwa zote zinaweza kurekebishwa lakini kwa kuzingatia maslahi ya walaji na watumiaji ambao ni wananchi na uchumi kwa ujumla," amesema kwenye hotuba hiyo.

Ameongeza kwa kutoa rai kwa vyombo vingine vya serikali vilivyohudhuria semina hiyo ikiwemo TFDA, TBS, BRELA, TAFFA, TPSF, CTI na Maofisa biashara wa wilaya na mikoa kuangalia namna bora ya kushirikiana na wafanyabiashara, wenye viwanda katika kutekeleza sheria zinazohusu usimamizi wa soko nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Mduma, amesema semina hiyo ni katika kutekeleza azma ya tume hiyo ya kuwaelimisha wadau mbalimbali kupitia vyama na jumuia zinazowaunganisha juu ya shughuli inazozifanya kisheria ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji wa pande hizo.

Amesema wanatarajia kuitumia semina hiyo kushauriana na wadau na kuelekezana kuhusiana na masuala mbalimbali ya udhibiti wa bidhaa bandia, ili kuimarisha mahusiano chanya  ambayo ni muhimu kwenye usimamizi wa shughuli za kibiashara katika mfumo wa uchumi na soko.

Dk. John amesema pia ili kuwa karibu zaidi na walaji, wameamua kuweka wazi namba ya simu ya bure, ambayo jana ilizinduliwa rasmi, itakayokuwa maalumu kwa wateja kuishauri FCC au kulalamika juu ya changamoto za sokoni.

Namba hiyo ni 0800110094.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: