Advertisement |
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imezuru mkoani Kagera na kuridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi (BBK).
Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imetembelea maeneo hayo ili kuangalia kazi za uhifadhi zinazofanywa, ambapo wameipongeza TAWA kwa kitendo cha kurudisha uasili wa mapori hayo, hali iliyosababisha kurejea kwa wanyamapori na uoto wa asili.
Wakizungumza mkoani humo jana, wajumbe wa kamati hiyo ya bunge walisema awali mapori hayo yalikuwa yameharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na makundi ya mifugo kufanya malisho katika maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nape Nnauye alisema ameridhishwa na masuala ya uendeshaji wa mapori hayo huku akiahidi kusaidia serikali kwenye ushauri, ili iweze kuwekeza miundombinu itakayokuza utalii katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Tunatambua kuwa TAWA ni changa haijaanzishwa muda mrefu lakini ndani ya kipindi kifupi imeweza kufanya mambo mazuri katika kulinda Maliasili zetu , Sisi kamati tumeridhisha na utendaji wake,’’ alisema Nape.
Alisema kutokana na utendaji kazi mzuri wa mamlaka hiyo, wataishauri na kuishawishi Serikali iongeze fedha katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ili iweze kutimiza wajibu yake kikamilifu zaidi.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla aliielezea kamati hiyo kuwa TAWA ipo mbioni kubadili mfumo wake katika mapori hayo.
Alisema moja ya mipango, TAWA badala ya kuendelea kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii pekee, imepanga kuanzisha utalii wa picha ili kufungua fursa za kiuchumi katika ukanda huo.
Waziri huyo alisema kutokana na mapori hayo kurejea katika uasilia wake baada kuharibiwa kwa kiasi kikubwa na uvamizi wa mifugo, hali iliyosababisha wanyamapori kuhama, Wizara inafanya utafiti ili kuongeza baadhi ya wanyamapori katika mapori hayo ili kuweza kuwavutia watalii wengi zaidi.
Awali kamati hiyo ilipokea taarifa kutoka kwa Wenyeviti wa Kamati za ulinzi na usalama za wilaya, ambapo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza ni uvamizi wa maeneo ya mapori ya akiba kwa kuanzisha shughuli za kilimo pamoja na kulisha mifugo ndani ya hifadhi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TAWA, James Wakibara, alisema moja ya mikakati ya TAWA ni kubadilisha aina ya biashara kwa kuanza kuchanganya ambapo TAWA itaendesha biashara ya uwindaji wa vitalu pamoja na utalii wa picha katika mapori hayo kwa lengo la kuiongezea serikali mapato
Alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha miundombinu kwa kuanza na barabara ndani ya mapori hayo ili kuweza kuwavutia wawekezaji kujenga hoteli mbalimbali ambazo watalii watazitumia kwa ajili ya kupumzika.
0 comments: