Advertisement |
KAMPUNI ya mradi wa Mabasi
yaendayo Haraka (DART), imesema ipo mbioni kutafuta muarobaini wa tatizo la
mafuriko kwenye karakana yake ya Jangwani, Dar es Salaam.
Kauli hiyo ilitolewa
jana jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare, alipozungumza
na gazeti la Uhuru ofisini kwake.
Lwakatare alisema
wakati wanajenga karakana hiyo, walichukuwa tahathari ili kama yakitokea mafuriko
yasiweze kuharibu miundombinu hiyo iliyogharimu serikali fedha nyingi.
Alitoa kauli hiyo,
katika wakati ambao gazeti la Uhuru limeshuhudia maji yakiwa tatizo kwenye eneo
ilipo karakana hiyo, kila unapotokea msimu wa mvua.
“Serikali ipo mbioni kutafuta
ufumbuzi wa tatizo lililopo katika karakana ya Jangwani na tunazo njia mbadala
za kufanya kwenye usanifu ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili,” alisema
Lwakatare.
Pia alisema licha ya
kwamba mvua za misimu ya mvua huleta athari katika karakana hiyo, bado
haijahamishwa kama taarifa kadhaa za upotoshaji zilivyodai na kusambazwa kwenye
mitandao ya kijamii nchini.
“Shughuli za DART
zinaendelea kama kawaida kwenye karakana yetu ya Jangwani,” alisisitiza.
Kuhusu mwendelezo wa
ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (BRT), kutoka Kamata,
Kariakoo mpaka Mbagala, Mtendaji huyo alisema, ujenzi wake bado haujaanza
lakini unatarajiwa kuanza muda wowote ndani ya mwaka huu.
Imeandikwa na Hamida Said
0 comments: