Advertisement |
Kitendo cha elimu kuonekana kuwa changamoto mkoani Lindi, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa jumla ya Sh. Bilioni 2.8 kuhakikisha mkoa huo unashika nafasi za juu kitaifa kwenye ngazi zote.
Mbali na fedha hizo ambazo kimsingi ni za programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), wadau mbalimbali wa elimu mkoani humo akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamedhamiria kufufua hadhi ya mkoa huo kitaaluma.
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi, ambaye amesema atahakikisha mkoa wake unapanda kitaaluma hasa ikizingatiwa tayari Program za EP4R na KKK zimeonyesha njia na kupokewa vizuri na baadhi ya wananchi wa Lindi.
Amesema mkoani hapa kuwa, faida za kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia shuleni ni nyingi na kwamba serikali inalitambua hilo hivyo kuhimiza wananchi kuunga mkono jitihada hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Zambi ametolea mfano shule ya msingi Mnacho, iliyopo wilayani Ruangwa, ambayo ndipo aliposomea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa awali kabla ya ukarabati, ilikuwa na hali mbaya kiasi cha kutaka kuifunga.
"Tunaishukuru serikali kwa program zake za EP4R na KKK, ambayo inahimiza ufahamu wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa hatua za awali shule za msingi, imeonyesha njia ya wengine kufuata katika suala zima la maboresho ya miundombinu ya shule," amesema.
Amesema licha ya kwamba ukarabati huo wa Mnacho haukuwa wa program ya EP4R, hali iliyopo shuleni hapo kwa sasa kama ilivyoelezwa na Mwalimu Mkuu, Theodensia Lukanga, imethibitisha kuwa juhudi za wadau binafsi kuisaidia serikali kwenye ukuaji wa sekta ya elimu zinawezekana.
Mwalimu huyo amesema shule hiyo ilikarabatiwa kwa msaada wa wadau mbalimbali, wakishirikiana na Waziri Mkuu Majaliwa, Mkuu wa mkoa na uongozi wa serikali ya kijiji na kata, hatua iliyoifanya ionekane mpya.
Amesema kwa ukarabati huo, wanafunzi wamepata hamasa kubwa kitaaluma na kuiomba serikali iendelee kuwatazama kwa jicho la tatu, hasa kuhusu upatikanaji wa walimu wanaokidhi uhitaji wa shule hiyo yenye historia ya kutoa kiongozi wa juu wa nchi.
Shule hiyo ya Mnacho ni moja kati ya shule za msingi mkoani Lindi, ambazo ukarabati wake haukuhusisha mradi wa EP4R lakini juhudi za wadau zimeifanya iwe na hali nzuri inayotoa fursa nyingine ya kuandaa viongozi wengine wa kitaifa na kimataifa kwa kipindi kifupi kijacho.
0 comments: