Advertisement |
Miaka takriban 20 iliyopita, Tanzania bado ilikuwa kwenye dunia ambayo linapokuja suala la kutumia maendeleo ya teknolojia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi, ilikuwa ndoto isiyojulikana kama itakuja kutimia au itabaki kuwa ya kusadikika kwa miaka mingi ijayo.
Kitendawili hicho kiliendelea kuumiza vichwa vya wataalamu wa uchumi hapa nchini na wananchi kwa ujumla pale waliposikia nchi zingine zinapiga hatua kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano kukuza mzunguko wa fedha hivyo kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi.
Ni kwa kiu hii, miaka 10 baadaye Tanzania iliamka na kuanza kutumia teknolojia kwa kuangalia namna ambavyo mawasiliano ya simu za mkononi yatatumika pia kufanya miamala ya fedha, huduma zilizoanza rasmi mwaka 2007 na kampuni iliyojulikana kama E-Fulusi chini ya huduma yake ya Mobipawa.
Wazo hilo kwa mujibu wa tafiti za IMF kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lilikuja baada ya kuona maeneo mengi hasa ya vijijini bado yalikuwa hayajafikiwa na taasisi za kibenki hivyo huduma za kutunza, kutunza na kutoa fedha zilikuwa bado kwa mfumo wa kizamani.
Mifumo hii ya kizamani naweza kuielezea kwa kukumbushia utumaji wa fedha kwa mabasi yaliyokuwa yakitoka sehemu moja kwenda nyingine huku mtumaji akilazimika kumlipa fedha kidogo dereva wa basi husika ili fedha zile zifike salama. Ilikuwa ni hatari sana.
Aidha, utunzaji wa fedha chini ya mto wa kulalia, chini ya ardhi, kwenye vyungu na maeneo mengine ya hatari ilikuwa mitindo ya kawaida ambayo kiuhalisia usalama wa fedha haukuwa na viwango hata walau kwa asilimia 0.01, muda wowote fedha zilikuwa zinapotea.
Leo ni miaka 10 baada ya kuanza rasmi kwa matumizi ya mfumo wa kutumia mitandao ya simu za mkononi kufanya huduma za kibenki yaani kutunza fedha, kutoa na kutuma kwenda kwa mtumiaji mwingine wa simu maeneo yote nchini kwa ada kidogo ili kufidia gharama za uendeshaji.
Wakati nazungumza haya, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2007 chini ya mtoa huduma mmoja (E-Fulusi), watanzania waliokuwa wamejisajili kwa ajili ya kutumia huduma ya Mobipawa walikuwa 112,000 lakini mwaka 2008, ambao ni mwaka mmoja baada ya kuanza rasmi kwa huduma hiyo walifika watumiaji 5300.
Ongezeko hilo kubwa la watumiaji ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, lilitokana na mitandao mingine ya simu kuanzishwa hapa nchini na mara moja kuanza kutoa huduma za kibenki kwa kutumia simu za mkononi.
Miongoni mwa kampuni za simu zilizojitosa kwenye soko la ushindani wa kutoa huduma za kibenki nchini ilikuwa ni Vodacom iliyoanza rasmi mwaka 2008 kwa huduma yake ya M-PESA, Milicom chini ya huduma yake ya TIGO PESA ikaingia mwaka 2009 na mwaka 2010, Airtel na Zantel zikaanzisha AIRTEL MONEY na EZY PESA.
Kampuni hizi ili kuendelea kufanya biashara zililazimika kufanya ubunifu ili kuvutia wateja walioanza kumiminika kwenye huduma hizi za miamala ya kibenki kupitia teknolojia za kisasa zinazotumiwa na kampuni za simu za mkononi hivyo kusababisha namba ya watumiaji kutoka 53,300,000 mwaka 2008 hadi kufikia watumiaji hai 17,600,000 Februari 2016.
Moja ya ubunifu uliotumiwa na kampuni hizi za simu ni kuanzisha huduma za mawakala, lengo likiwa ni kutanua wigo wao wa kufanya biashara ambapo kwa ufatifi uliofanywa mwaka 2015 na Benki Kuu ya Tanzania, hadi Februari 2016 walisajiliwa mawakala 260,000 nchi nzima.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2017 kuhusu uchumi inayotolewa na Benki ya Dunia, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kutokana na kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi wa huduma za miamala ya kifedha kwa simu za mkononi ukanda wa Afrika mashariki.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa mchango wa serikali chini ya BoT kwenye kusimamia usalama wa miamala ya fedha kupitia kampuni za simu za mkononi umekuwa siri kubwa ya mafanikio ya kukua kwa sekta ya mawasiliano.
Imezitaja sheria zinazosimamiwa na BoT ikiwemo ile ya 2006 kuwa ilitoa mamlaka kwa taasisi hiyo kubwa ya kifedha nchini kufuatilia kila muamala wa kibenki unaofanywa na taasisi zisizo na leseni za kutoa huduma za kibenki hivyo kuepusha hatari ya usalama wa fedha za watu kuwa ndogo.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chrispin Rutta, anasema ujio wa teknolojia ya miamala ya fedha kwa simu imetoa nafasi kwa watanzania kutumia huduma za kibenki bila kuathiri uchumi wala biashara za benki nchini.
Anasema watu wengi hufikiri kuwa benki zinapata hasara kutokana na uwepo wa huduma za kutunza, kutuma na kupokea fedha kutoka kwenye simu za mkononi lakini hakuna ukweli katika hilo kwa sababu kampuni husika hazina leseni ya kufanya biashara ya benki kutoka BoT.
"Hawa watu mitandao ya simu wao hawana leseni zile ya BoT zinazowaruhusu wafanye biashara ya benki, hivyo wana akaunti kwenye benki hizo hizo wanazosema watu zinapata hasara kutokana na uwepo wa Airtel Money, Mpesa, Halopesa na nyingine," anasema.
Mchumi huyo anasema kwa utafiti aliowahi kuusoma kwenye tovuti ya BoT, Tanzania hadi kufikia Septemba 2016, asilimia 75 ya watu wote wana miliki akaunti za simu zenye uwezo wa kutuma na kupokea simu huku asilimia 14 tu ndio wenye umiliki wa akaunti za benki.
Anasema kwa takwimu hizo, uhalisia ni kwamba teknolojia ya simu kutumika kama akaunti ya benki huku ikitoa pia huduma za mikopo yenye riba, imetoa mchango mkubwa kwenye maeneo yote ya mijini na vijijini kwa watumiaji kuwa na shughuli binafsi za kujiingizia kipato hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi.
"Unaweza kuona sasa hivi badala ya vijana wengi kulalamika hakuna ajira, wameajiriwa kama mawakala wa simu hizi wanatoa na kuingza fedha na kupata asilimia zao kwa huduma ile jambo linalowapa kipato cha kuendesha familia zao, kiuchumi haya ni maendeleo makubwa sana," anafafanua.
Mmoja wa watoa huduma kwenye moja ya benki za biashara hapa nchini, anasema miamala ya kibenki kwa siku za hivi karibuni imekuwa ikiongezeka zaidi kutoka kwenye simu za mkononi ikilinganisha na miamala ya kawaida ya kibenki hasa kutokana na ubia uliopo baina ya kampuni za simu na taasisi za kibenki.
"Leo mtu anaweza kuingia kwenye akaunti yake ya CRDB au NMB au benki yoyote kutoka kwenye simu yake na kutoa kiasi fulani cha fedha kisha kuzihamishia kwenye akaunti yake ya simu akiwa popote hata kama hakuna tawi la benki husika, mambo ni rahisi uchumi unasonga mbele," anasema Calvin Tillya.
Hata hivyo anasema bado kuna umuhimu wa kuwa na akaunti benki ni muhimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo usalama zaidi wa fedha na faida kwa fedha za mmiliki wa akaunti lakini pia kwa sababu za kiuchumi za mzunguko wa fedha kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine au sekta moja kwenda nyingine.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wao kwa nafasi yao wanasema wanaendelea kufuatilia mienendo ya kampuni zote za simu kuhakikisha kuwa kila mtoa huduma anafanya sawa na mkataba wake alioingia na serikali.
"Hatutaki mtoa huduma yeyote afanye shughuli zake hapa nchini kinyume na mkataba wake na sisi, fedha ni mali ya serikali hivyo shughuli zote zinazozihusu zinatakiwa kusimamiwa ili kuepuka zisitumiwe vibaya ikiwemo masuala mazima ya kiuhalifu, TCRA tuko makini katika hili," anasema
Francis Kopwe ambaye ni mtaalamu ICT kutoka mamlaka hiyo.
Kwa upande wao wananchi waliopata fursa ya kuzungumza kwenye makala hii, wanasema huduma za fedha kwa simu zimekuwa mkombozi wa masuala yao muhimu ya kifedha na kwamba wanatamani ada za kulipia gharama za uendeshaji zipungue kidogo tofauti na ilivyo sasa.
Wanasema kwa watu wachache waliopo ambao wanajaribu kutumia ujanja kuiba fedha za watu kwenye akaunti za simu, TCRA na mamlaka zingine zinapaswa kuangalia namna ya kudhibiti zaidi ili faida ziendelee kuwa nyingi zaidi kwenye ukuaji wa uchumi ikilinganishwa na hasara.
Nao baadhi ya wafanyabiashara walioona fursa ya kuwa mawakala wa miamala ya fedha kwa simu za mkononi akiwemo Ramadhan Sule wa Chanika, wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, anasema anamiliki akaunti za kampuni tatu za simu ambapo kwa wastani kila siku kwenye tigopesa anapata wateja wasiopungua 150 huku Airtel Money na Mpesa wakifika zaidi ya 200 jambo linalompa faida kubwa katika kuendelea kiuchumi na familia yake.
Kiuhalisia miamala ya fedha kwa simu za mkononi imeshika hatamu hapa nchini, mtu anaweza kumiliki akaunti tano za kufanya miamala ya kifedha kutoka kwenye kampuni tano tofauti za simu za mkononi lakini akawa na akaunti moja kutoka kwenye taasisi moja ya benki.
Hivi karibuni nimesikia TTCL nao wanataka kuanzisha huduma ya kifedha kama zilivyo kampuni zingine za kifedha, hii ni hatua nzuri hasa ukizingatia ni taasisi ya umma kwa asilimia zote ukiitofautisha na kampuni zingine za simu zinazomilikiwa na watu binafsi hivyo naamini itatosha ushindani mzuri wa haki.
Mbali na hilo, kampuni mbalimbali na mashirika likiwemo la ugavi wa umeme (TANESCO), majitaka na majisafi Dar es Salaam (DAWASCO) na nyingine nyingi zimeamua kushirikiana na teknolojia za kampuni za simu ili kulipia ada za matumizi ya huduma zao kokote jambo linaloongeza umuhimu wa huduma hizo za miamala ya fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Ni ukweli usiopingika kwamba uchumi wa nchi hukua kwa mchango wa kila mwananchi, teknolojia imerahisisha mambo hivyo ni vyema watanzania wakaitumia vizuri hususan kwenye suala zima la kufanya miamala ya kibenki kwa namna salama huku wakitunza namba zao za siri kwa usalama wa fedha zao.
0 comments: