Advertisement |
Majambazi watatu wanaotuhumiwa kuliteka basi la Safi na, kupora fedha, simu na kuwatandika viboko abiria katika Mlima Rogea, wilayani Chunya, Mbeya wametiwa mbaroni.
Imeelezwa kuwa majambazi hayo matatu kati ya sita, yaliyoshiriki tukio hilo, yametambuliwa na abiria, baada ya kukutwa yakiwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 388 BFZ, waliyoitumia kwenye tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema baada ya tukio hilo la uporaji, polisi walifanya msako mkali na kufanikiwa kuwatia mbaroni majambazi hayo matatu.
Mpinga aliwataja watuhumiwa wa ujambazi kuwa ni Juakali Mbalamwezi (65) na Gaspar Mahini (22), wakazi wa Sumbawanga na Petro Juma (21) mkazi wa Chunya.
Alisema abiria kadhaa walipata michubuko na mikwaruzo na walipatiwa matibabu katika zahanati ya Makongolosi na kuruhusiwa baada ya kuonekana hali zao zinaendelea vizuri.
“Mara baada ya kufanya tukio hilo la utekaji na kisha kuwapora abiria, majambazi hayo yalifyatua risasi hewani na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia usafi ri wa pikipiki,” alisema Mpinga.
Katika hatua nyingine, Mpinga amewatakia Heri ya Sikukuu ya Eid El Haji, wakazi wa mkoa wa Mbeya na kuwataka washerehekee kwa amani na utulivu, huku wakizingatia sheria, kanuni na utaratibu wa nchi.
“Watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara, ni vyema wazingatie sheria za usalama barabarani” alisema Mpinga.
0 comments: