Advertisement |
Kiungo wa pembeni wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amewasili kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana, utakaochezwa Septemba 1, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Msuva aliwasili Dar es Salaam jana kutoka Morocco anakocheza timu ya Diffaa el Jadida na ataungana na kikosi hicho katika mchezo huo uliopo katika Kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema Msuva aliwasili na Ndege ya Shirika la Kenya (KQ), kutoka nchini Morocco.
Ofisa huyo alisema Msuva amechelewa kuwasili nchini kwa kuwa alikuwa akifuatilia hati ya kusafi ria ya muda mrefu.
Alisema mchezaji huyo alianza mazoezi na wenzake jana jioni na leo Taifa Stars itafanya mazoezi ya mwisho asubuhi kabla ya kuikabili Botswana kesho.
“Msuva ameshawasili nchini akitokea Morocco kwa mchezo dhidi ya Botswana, mchezaji wa kulipwa atakayekosekana ni Morel Organes anayeichezea Famalicao ya Ureno, kufuatia kukosa kibali cha kutoka nchini humo,” alisema Lucas.
Wachezaji wengine wanaounda kikosi hicho wanaocheza soka la kulipwa ambao waliwasili ni Farid Mussa (Tenerrife, Hispania), Abdalah Hamis (Sony Sugar, Kenya), Elius Maguri (Dhofar, Oman) na Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini) na nahodha Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji.
Wengine ni makipa, Aishi Manula (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Ramadhani Kambwili (Yanga).
Mabeki: Gadiel Michael (Yanga), Boniface Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba) na Erasto Nyoni (Simba).
Viungo: Himid Mao (Azam), Mzamiru Yassin (Simba), Said Ndemla (Simba), Shiza Kichuya (Simba), Rafael Daud (Yanga) na Kelvin Sabato (Azam).
Katika mchezo huo, timu itakayoshinda itapanda katika ubora wa viwango vinavyotambuliwa na FIFA.
0 comments: