Thursday, June 1, 2017

MAKALA - Mazingira

ad300
Advertisement

Majanga ya asili yanaepukika kwa kutunza vyanzo vya maji


NA WILLIAM SHECHAMBO
Licha ya kwamba maji ni muhimu kwa maendeleo ya afya ya mwanadamu, wanyama na mimea lakini pia ni rasilimali muhimu katika maisha ya kila siku ya kiumbe hai yeyote.

Umuhimu wa rasilimali hii unakwenda mbali zaidi kwa sababu sekta mbalimbali zenye mchango chanya kwa maendeleo zinategemea maji hasa kwenye suala zima la upozaji wa mashine za viwandani, uzalishaji wa nishati ya umeme bila kusahau uchukuzi wa baharini, ziwani na mito.

Kwa upande wa sekta ya utalii, inategemea pia maji kupata maporomoko ya kufutia macho, kuhuisha mimea na wanyawapori ili wawe na afya, wazidi kuzaliana na kuongezeka jambo linalowavuta wageni kutoka kila kona ya dunia kutalii.

Ulinzi wa bayonuai kwa kiasi kikubwa unapewa uwezo na uwepo wa maji kwenye eneo husika, kwa sababu kama wahenga walivyosema maji ni uhai, ndivyo kiuhalisia ilivyo hivyo rasilimali hii ni mtambuka kwa ustawi wa sekta zote.
Hata hivyo licha ya umuhimu wake, watu wamekuwa na matatizo makubwa kwenye matumizi yake, hivyo kusababisha uhaba kwenye maeneo mbalimbali unaotokana na uharibifu  wa vyanzo vya maji yakiwemo mito, chemchemi na mabwawa.

Matatizo ninayoyazungumzia hapa ni kwenye utunzaji, ambapo kwa muda mrefu mbali na kutolewa kwa elimu ya utunzaji wa vyanzo hivyo, bado kumekuwa na migogoro mikubwa kati ya watumiaji wa maji kwenye mazingira hasa wakulima, wafugaji.

Hilo limekuwa donda ndugu ambalo bila hiyana linaendelea kutafuna jamii za maeneo mengi na kusababisha ukame kwenye mazingira yao hali inayosababisha kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mantiki hii, watu wanapaswa kujua kuwa utunzaji wa rasilimali za maji ni suala la kufa na kupona; likitegemea sana upatikanaji, matumizi na usimamizi wake.

Denis Kiilu, Ofisa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, anasema kutokana na uzoefu wake kwenye kutembelea maeneo mbalimbali, ni wazi kuwa maji yakiwa machache au yakichafuliwa yanaweza kusabisha uharibifu, majanga, umasikini na hata vifo.

Anasema kwenye maeneo mengi, hali hiyo inaweza kuzorotesha maendeleo ya kiuchumi ya eneo husika na nchi kwa ujumla kutokana na athari za kiafya, uhaba na usalama mdogo wa chakula.

"Kila mara Wizara tunasisitiza kuwa kama rasilimali hii ikitumiwa vyema, ni kichocheo katika ukuaji wa uchumi, kuondoa umasikini na kupunguza matatizo ya huduma ya majisafi na salama na usafi wa mazingira lakini bado kunaonekana kuna shida mahali," anaeleza.

Ofisa huyo anaongeza kuwa pamoja na umuhimu wa maji, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji hapa nchini, ambapo chanzo kikubwa cha tatizo ni shughuli za kibinadamu ambazo kwa kiasi kikubwa zimesababisha athari nyingi zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ukame na mafuriko.

Anasema kwa uchunguzi alioufanya, uharibifu wa vyanzo vya maji unachangiwa na uchafuzi wa maji, unaotokana na umwagaji wa maji machafu kwenye vyanzo hivyo kutoka viwandani, migodini na nyumba za watu hivyo kusababisha magonjwa ya kipindupindu, kuhara na saratani.

Sababu nyingine ni uchukuaji au uchepushaji wa maji mengi kutoka kwenye vyanzo vya maji vilivyo juu ya ardhi ikiwemo mito kuliko uwezo wa vyanzo hivyo, na kusababisha uharibifu wa mazingira, matumizi holela ya ardhi yanayopunguza udongo wenye rotuba na uoto wa asili, hivyo kubadili mfumo wa maji wa kusafiri na kuvia kwenye ardhi.

Mbali na sababu hizo, anasema kuenea kwa mimea isiyo asili kwenye vyanzo vya maji pia kunachangia uchafuzi wa maji na uharibifu wa bionuwai, huku shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji na usafishaji madini ndani au kandokando ya vyanzo vya maji ukiongoza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa maji kwa kuyaweka kemikali zenye sumu na madhara kwa binadamu na viumbe hai vingine.

Anasema madhara ya kuharibu vyanzo vya maji, yana mfano hai kwenye Mto Ruaha Mkuu kati ya kipindi cha mwaka 1994-2000, ambako kulikuwa na ongezeko kubwa la muda ambao mto huo ulikuwa ukikauka wakati wa kiangazi kutoka mwezi mmoja miaka iliyopita hadi miezi mitatu, kutokana na ongezeko la matumizi ya maji kwa shughuli mbalimbali zinazofanyika katika eneo la juu la mto.

Ofisa huyo anasema kukauka kwa mto huo kulivuruga maisha ya viumbe na wanyamapori wengine katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kauli iliyothibitishwa na Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk. Christopher Timbuka.

Dk. Timbuka anasema mto huo ndio chanzo kikuu cha maji ya kulishia wanyamapori ndani ya hifadhi hiyo yenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba na makundi makubwa ya tembo ambapo kila tembo anakunywa maji lita 200 kwa siku.

Uchunguzi umebaini kuwa matumizi mabaya ya ardhi kandokando ya mito na kwenye miteremko ya milima huchangia kupotea kwa uoto wa asili na udongo wa juu ambao ndio hasa wenye rotuba kwa kilimo kizuri. Hii husababisha ongezeko la mmomonyoko wa udongo, kama ilivyo katika eneo la Bonde la Mto Soni, wilayani Bumbuli, ambako kuna mrundikano mkubwa wa mchanga kwenye mto.


Rekodi zinaonesha kuwa kiasi cha zaidi ya mita tatu za udongo ziliwahi kurekodiwa katika banio na mfumo mzima wa umwagiliaji wa mto huo, ambapo kulisababisha mafuriko ya mwaka 1991 yaliyofanya watu kadhaa kupoteza maisha na uharibifu mkubwa kutokea wakati eneo hilo likiwa Wilaya ya Lushoto kabla ya kugawanywa.

Majanga ya asili kama ukame na mafuriko yanapotokea huleta madhara kwa jamii na hasara kubwa kiuchumi. Majanga haya ambayo kimsingi chanzo chake ni ni mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa hutokea kutokana na kupungua kwa maji kwenye mito na vina vya maji kwenye mabwawa.

Madhara yake yakiwemo kupungua kwa mazao, ubora wa maji, usalama wa chakula, uzalishaji umeme unaotokana na maji, na kuongezeka kwa matumizi ya maji yaliyo chini ya ardhi, kunasababisha hatari ya kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai na hugusa watumiaji maji waishio ndani na nje ya maeneo yenye vyanzo vya maji.

Aidha kuna uhusiano mkubwa kati ya maji, ardhi, mazingira pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa hiyo hatuna budi kuweka mikakati sahihi ya kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali zetu, ili kujilinda madhara yaletwayo na majanga ya asili yanayotokana na shughuli za kibinadamu.

Hivyo basi, hatuna budi kuwa na mikakati madhubuti ya kuendeleza Sekta ya Maji itakayotuwezesha tuwe na usalama wa chakula, kupunguza umasikini na tuwe na mazingira salama.

Kila mtu ana nafasi kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji, hakuna sababu ya kuacha maji yamwagike chini bila sababu za msingi kwani ni mali ya thamani kubwa pale inapokosekana, timiza wajibu, maji ni uhai.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: