Advertisement |
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo amezindua bodi ya ushauri ya wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) ambapo ameitaka bodi hiyo iisaidie ADEM kutimiza majukumu yake ipasavyo kwa upande wa kutoa mafunzo, nidhamu ya utendaji kazi na kusimamia vyema matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya Taasisi hiyo.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo Februari 3 Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa anategemea kuona matokeo chanya kutoka kwenye bodi hiyo kwa kuwa wote walioteuliwa wamebobea katika masuala mbalimbali yanayohusu Elimu.
Akizungumza mara baada ya maelekezo ya Waziri, Mwenyekiti wa bodi hiyo Dk.Naomi Katunzi amemhakikishia Waziri Ndalichako kuwa bodi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Dk. Katunzi amesema kuwa wamepokea kwa mikono miwili uteuzi huo na kuwa watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu Kati ya bodi na uongozi wa ADEM.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Dk. Siston Masanja amesema bodi hiyo itaishauri ADEM katika masuala mbalimbali ili kufikia malengo yanayokusudiwa.
Wajumbe wa bodi hiyo ni Dk. Siston Masanja ,Mick Kiliba, Dk. Eugenia Kafanabo, Dk. Christina Raphael, Dk. Ernest Mwasalwiba, Gerald Mweri na Mwanyika Semroki.
Bodi hiyo ambayo imezinduliwa leo itatekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka Mitatu.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.
3/2/2018
0 comments: