Advertisement |
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Hamis Kigwangallah amesema hatajibu maombi yoyote yaliyowasilishwa ofisini kwake kutoka kwa walio chini yake, ambayo yanayohusu kufuta maeneo ya Hifadhi ili yatumike kwa ajili ya matumizi mengine.
Amesema maeneo hayo yalitengwa kisheria na yana umuhimu mkubwa kiuchumi na kijamii hivyo lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho hivyo mwenye mamlaka ya kumfanya abadili uamuzi huo ni aliyemteua pekee.
"Katika kipindi cha Uwaziri wangu, sitajibu ombi lolote lile linalohusu kubadili matumizi ya maeneo hayo kwa vile kuwa na misitu sehemu za mijini ni sehemu ya maendeleo," alisema.
Aliyasema hayo mjini Iringa alipokuwa akizungumza kwa mara ya kwanza na kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu iliyokutana kwa ajili ya kufanya kikao chake cha tatu tangu ilipoundwa mwaka jana.
Hatua hiyo iliambatana na kutembelea msitu wa Hifadhi wa Kihesa Kilolo uliiombwa na uongozi wa mkoa kufutwa ili upate kutumika kwa kuweka miundo mbinu mipya ya mji wa kitalii.
Katika kikao hicho ambacho Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alishiriki, Waziri Kigwangallah aliyeambatana na Naibu waziri wake, Japhert Hasunga alimuomba Mkuu huyo awafikishe ujumbe Wakuu wa mikoa wengine ambao walituma na wanaotarajia kutuma maombi ya namna hiyo kuwa yeye hatayajibu hadi pale aliyemteua atakapompa maelekezo na si vinginevyo.
Alisema halmashauri nyingi nchini kila zikiona maeneo ya Hifadhi zimekuwa zikifikiria kubadili matumizi ya maeneo hayo ili yatumike kwa shughuli zingine za maendeleo kama vile kupima viwanja ili kuwauzia wananchi kwa lengo la kukusanya mapato.
"Ofisini kwangu kuna maombi mengi mno ambayo hata sielewi nianze na lipi na niache lipi, nasema sitajibu ombi lolote lile" alisisitiza Waziri Kigwangallah.
Aidha, Waziri Kigwangallah mara baada ya kuzungumza na kamati hiyo alitembelea eneo la hifadhi ya msitu huo huku akiwa ameongoza na kamati hiyo pamoja na Uongozi wa Mkoa wa huo.
Wakati akitembelea eneo hilo, Waziri Kigwagwallah aliwashangazwa na kitengo cha viongozi wa halmashauri kuanzisha dampo katika eneo hilo huku kamati ikijionea magari matatu ya taka yakiendelea kumwaga uchafu kwenye eneo hilo jambo ambalo ni kinyume na sheria za uhifadhi.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Japhet Hasunga aliwashukia watendaji wa mkoa huo wakati walipokuwa wakipishana kutoa maelezo kuhusiana na mipaka na matumizi ya eneo hilo endapo Wizara itaridhia ombi lao la kubadili matumizi ya eneo hilo.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alimuhakikishia Waziri kuwa eneo hilo endapo watapewa litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Waziri Kigwangallah mara baada ya kutembelea eneo hilo wakati akitoa majumuisho yake, alisema kufuatia ziara hiyo anasubiri ushauri utakaotolewa na kamati ya kitaifa ya msitu ndipo atakapokuwa na jibu kuhusiana na ombi la kubadilia matumizi la eneo hilo .
Pia, Waziri Kigwangallah aliiagiza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuwa maeneo ya milima kwa vile sio moja ya maeneo ya hifadhi yaongezwe katika eneo la hilo lengo likiwa ni kuzuia uharibifu wa uoto wa asili unaoendelea katika maeneo hayo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati akitoa neno la shukrani alimhakikishia Waziri kuwa watamshauri jambo lolote lile linalohusu misitu bila kujali litamfurahisha au litamuudhi, kitakachoangaliwa hapo ni maslahi mapana ya taifa.
Katika hatua nyingine ,Waziri Kigwangallah ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kuanza kuweka nguvu nyingi katika kuhifadhi misitu baadala ya kuvuna na kufanya biashara ya mazao ya misitu.
Alisema licha ya kuwa TFS imekuwa ikifanya vizuri katika baadhi ya maeneo lakini katika suala la kuhifadhi misitu imekuwa kama vile sio kazi yake: "TFS yenyewe kazi yake imekuwa ni kuvuna kilichopandwa, kuuza na kukusanya mapato yatokanayo na mazao ya misitu" alisema.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangallah amesema Wizara inakusudia kuchukua misitu yote iliyo chini ya vijiji na Halmashauri kwa vile zimeshindwa kuisimamia ipasavyo na hivyo kupelekea sehemu kubwa ya nchi kugeuka kuwa jangwa.
Mbali na hilo amewaonya wananchi wanaowazuia watendaji kuweka alama za vigingi katika mipaka ya hifadhi, huku wengine wamekuwa wakiving'oa na wengine kuhamisha vigingi hivyo kutoka eneo moja hadi jingine kuwa waache tabia hiyo kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.
0 comments: