Monday, August 28, 2017

Ujenzi kivuko kipya cha Kigongo Busisi waanza

ad300
Advertisement

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dk. Mussa Mgwatu, ameshiriki katika zoezi la kuweka msingi wa ujenzi wa kivuko kipya kitakachotoa huduma ya usafiri katika Ziwa Victoria kati ya Kigongo na Busisi Mkoani Mwanza.

Zoezi hilo linaloashiria kuanza rasmi kwa ujenzi huo limefanyika Pasiansi katika eneo linalotumika kwa ajili ya ujenzi wa meli, vivuko na boti linalomilikiwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Limited ya Mwanza iliyoshinda zabuni ya kujenga kivuko hicho kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8.9 za kitanzania. 
Tukio hili la kihistoria lilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Ukodishaji Mitambo na Huduma za Vivuko kutoka TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle, Mhandisi Amos Mutahiwa kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bwana Salehe Songoro Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro, na wafanyakazi wa Kampuni ya Songoro na wale wa TEMESA.
Akiongea baada ya zoezi hilo, Dk. Mgwatu amesema wakazi wa Mwanza wana kila sababu ya kujivunia kuanza kwa ujenzi wa kivuko hicho kwani kitakapokamilika kitasaidia kurahisisha usafiri wa abiria na mali zao na hivyo kuimarisha uchumi wao. 
Dk. Mgwatu amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anamaliza kujenga kivuko ndani ya muda uliopangwa kwenye mkataba na kuzingatia ubora wa hali ya juu. 
Pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi ya vivuko kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri. 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati huku akisisitiza kuwa kampuni yake imejipanga vyema kufanya kazi kwa kasi kwa kuwa malighafi kwa ajili ya ujenzi wa kivuko tayari ipo kwenye eneo la ujenzi.
Kivuko hicho kipya kitakapokamilika kitafanya idadi ya vivuko vinavyotoa huduma katika eneo la Kigongo Busisi kufikia vinne vikiwemo vile vya MV. Sengerema, MV. Misungwi, pamoja na MV. Sabasaba.

Habari hii imeandikwa na:
Alfred Mgweno (TEMESA MWANZA)
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: