Thursday, August 3, 2017

Uhuru acharuka

ad300
Advertisement
Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ni mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee, amewaagiza polisi kuharakisha uchunguzi wa kifo cha Mkurugenzi wa TEHAMA wa Tume ya IEBC, Chris Msando, ili kuhakikisha kwamba waliohusika wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.

Uhuru alitoa maagizo hayo kwa  Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet, katika Uwanja wa 64, jijini Eldoret, ambapo aliambatana na naibu wake William Ruto, kwenye kampeni za lala salama za uchaguzi wa mwaka huu ambapo alisema ni lazima wanaohusika na mauaji hayo wapatikane.

Aidha kutokana na mauaji ya ofisa huyo wa IEBC, Rais Kenyatta aliwataka polisi waimarishe usalama kwa wagombea urais wote na wafanyakazi wote wa tume hiyo ya Uchaguzi.

“Niwawaomba polisi kuongeza usalama wa wagombea urais, wagombea wenza wao na wafanyakazi wa IEBC ili kuhakikisha kuwa majukumu yao hayaathiriwi kwa vyovyote vile,” alisema rais.

Alitoa kauli hiyo huku zikiwa ni siku kadhaa tangu nyumba ya Naibu wake, William Ruto ivamiwe na kutokea kurushiana risasi kwa saa 18 kati ya wanausalama na wavamizi ambao mpaka sasa bado hawajapatikana.

Rais Kenyatta kabla ya kuhitimisha kauli yake kuhusu tukio hilo la kusikitisha na baada ya kuomba kura ya ndio kwa wakazi hao, alisema anatoa pole kwa familia ya Msando, ndugu, jamaa, marafiki na wakenya wote kwa kumpoteza mchapakazi aliyejitolea kulitumikia taifa lake kwa uzalendo kwenye utekelezaji wa demokrasia.

Katika hatua nyingine, mjini Kisii, viongozi wa NASA nao wakizungumza na wapiga kura kwenye mikutano miwili tofauti ya kampeni, walitaka uchunguzi ufanywe haraka ili waliohusika wajulikane na kufikishwa mahakamani.

“Sisi kama NASA tunataka kujua ni akina nani waliohusika na kifo cha Msando na walikuwa na nia gani,” alisema Kalonzo Musyoka.

Mwili wa Msando ulipatikana ukiwa kando ya mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 21, ambapo vifo vyao pamoja na mambo mengine ya uchaguzi vinadaiwa kuhusishwa na wivu wa kimapenzi huku upelelezi wa kuwabaini wahusika ukiendelea kila kona ya nchi hiyo.

Uchaguzi wa Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: