Thursday, August 3, 2017

Tume ya uchaguzi yawatoa hofu wakenya

ad300
Advertisement
Tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya (IEBC), imeuhakikishia umma wa Kenya kuwa itaendesha uchaguzi wa huru na haki.

Kamishna wa tume hiyo, Dk. Roselyne Akombe, alisema jana kuwa kila kitu kipo katika hali nzuri ambapo watafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kutoa kile ambacho Wakenya wanakihitaji.

Dk. Roselyne alisema ni wazi kuwa wako katika kipindi kigumu baada ya kuondokewa na Mkurugenzi wa TEHAMA aliyeuawa na watu wasiojulikana lakini wamekula kiapo kuitumikia nchi hiyo katika jukumu zito lililo mbele yao.

"Licha ya mwenzetu Chris Musando kutuacha na ndiye alikuwa mtaalamu wa Teknolojia, bado tutafanya juhudi kuona ya kwamba uchaguzi unaendeshwa  kwa njia ya kumridhisha  kila mmoja," alisema Dk. Roselyne.

Alisema maofisa wa mawasiliano na Teknolojia waliobaki wana ujuzi wa kutosha wa kuendesha uchaguzi huru na wa haki na kwamba hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.

Kamishna huyo aliyasema hayo alipohojiwa na kituo cha runinga cha Citizen, jana jioni na kuwataka wananchi nchini Kenya kujiandaa kwenye siku chache zilizosalia.

Moja ya maandalizi ya mwisho aliyoyataja kutekelezwa na tume hiyo ni ukaguzi na majaribio ya mitambo ya kupigia kura ili kuhakikisha zote kipo tayari kwa kazi ambapo hata zikileta matatizo kutakuwa na njia mwafaka wa kurekebisha haraka.

Alisema kuhusu changamoto za uwepo wa maeneo ambayo mawasiliano si mazuri, yatashughulikiwa vilivyo ili kuona ya kwamba mawasiliano yanafika kwa uwazi bila kuchakachuliwa.

"Kila matokeo yatatolewa baada ya muda wa saa chache ili wananchi waweze kujionea wenyewe jinsi mambo yatakavyoendeshwa, tutakuwa wazi sana haijawahi kutokea," alisema.

...YAPOKEA KARATASI ZA KURA YA URAIS

Wakati huo huo, maofisa wa IEBC walisema wanatarajiwa kupokea shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura ya urais tayari kwa uchaguzi mkuu Jumanne wiki ijayo.

Karatasi hizo zilizotarajiwa kuwasilishwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ja jioni, zitakuwa kwenye vifurushi 161 na ni za kaunti kuanzia namba 31 hadi namba 47.

Awali, tume hiyo ilikuwa imepokea vifurushi 192 vya karatasi za kupigia kura za majimbo mengine 30.

IEBC inatarajiwa kupokea jumla ya karatasi 20,818,000, ambapo kuna karatasi za ziada takriban milioni moja.

Tume hiyo ilisema jana kuwa imeongeza jumla ya kura asilimia moja kila kituo kufidia karatasi za kura ambazo huenda zikaharibika wakati wa upigaji kura.

Baadhi ya wagombea walikuwa wanalalamikia idadi hiyo ya kura za ziada wakisema huenda ikatumiwa kuiba kura.

Lakini Kamishna Dk. Roselyn alipangua tuhuma hizo na kuwaondoa hofu kwamba sheria za uchaguzi zinamruhusu mpiga kura anayeharibu karatasi ya kura kabla ya kutumbukiza karatasi yake kwenye kifaa maalumu cha kutunzia kura kupewa karatasi nyingine.

"Akiharibu mara nyingine, anaweza kupewa tena karatasi nyingine. Hii ina maana kwamba kuna baadhi ya wapiga kura wanaoweza kutumia karatasi tatu za kura," alisema.

Mwanzoni mwa maandalizi ya uchaguzi huo, kulizuka utata kuhusu zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kura ya urais ambapo kesi ilifunguliwa na upande wa upinzani lakini Mahakama ya Rufani iliamua kampuni ya Al-Ghurair ya Dubai ichapishe karatasi hizo.

Jumla ya wapiga kura 19,611,423 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo mkuu wa Jumanne wiki ijayo.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: