Monday, July 17, 2017

TEHAMA ni chachu ya mapinduzi ya taaluma nchini

ad300
Advertisement
Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yana mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya elimu na taaluma kwa ujumla.

Hii ni sawa na kusema kuwa kutokana na dunia tuliyopo sasa, huwezi kuitenganisha elimu na teknolojia kwa sababu ya mwingiliano uliotokana na kukua kwa utandawazi kwenye kila pembe ya dunia.

Ili kulithibitisha hili wakati fulani mwanazuoni ambaye ni raia wa Uingereza aliwahi kusema kuwa teknolojia imekuja kufanya mapinduzi kwenye sekta ya elimu duniani na yule atakayekataa mapinduzi hayo atasalia kwenye karne ya 19 wakati wenzake wakisonga mbele.

Tanzania kama moja ya nchi kati ya nchi 197 duniani na mataifa 55 barani Afrika, inatambua umuhimu wa teknolojia kwenye maendeleo ya sekta hii nyeti kwa maendeleo ndio sababu katika kipindi cha miongo miwili yameonekana mabadiliko makubwa kwenye sekta ya elimu nchini.

Nikizungumzia mabadiliko haya, nalenga kwenye mafunzo ya walimu wa sekondari kwenye ufahamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yaani TEHAMA, kuanzishwa kwa maabara za kisasa za TEHAMA katika baadhi ya shule na uwepo wa mtaala wa somo hilo muhimu.

Wanafunzi wa sekondari kwenye shule zote zikiwemo za kata, imeshuhudiwa wakichagua kufanya mitihani ya Kompyuta kama moja ya mitihani ya kitaifa ya kuhitimu elimu ya sekondari na kufaulu kwa kiwango cha kuridhisha kwa mujibu wa matokeo ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).

Kutokana na hali hiyo, matokeo ya NECTA yanaonyesha kuwekuwa pia na ongezeko la wanafunzi wanaochaguliwa kidato cha tano kwa michepuo ya sayansi na kujiunga na taasisi za elimu ya juu kwa vitivo vya  sayansi ya TEHAMA katika miaka 10 iliyopita ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Si hayo tu, wanafunzi wengi hapa nchini kutokana na uchunguzi wa makala hii, imegundulika kuwa wanatumia kwa kiasi kikubwa mtandao wa intaneti kupakua masomo yao kabla ya kufundishwa na Mwalimu darasani ili kutoa ushirikiano kwa mwalimu pale anaupohitaji na mwanafunzi hurekebishwa kama amekosea kwani si kila taarifa za kwenye intaneti ni sahihi.

Licha ya mafanikio hayo, hivi karibuni serikali imechukua hatua iliyopongezwa na idadi kubwa ya wananchi ya kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kuwezesha wanafunzi wa kidato cha tano wa mwaka huu kupata taarifa za kujiunga na shule walizochaguliwa kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI.

Kwenye tovuti hiyo, Shule zote za umma kwa upande wa Tanzania Bara zenye kidato cha tano na sita zililazimika kuwasilisha taarifa muhimu za shule kwa mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga kuendelea na elimu yake kwa TAMISEMI tofauti na awali zilipokuwa zinapatikana shuleni.

Hasara ya wanafunzi kupata taarifa hizo 'Joining Instruction' moja kwa moja kutoka shuleni kwa mujibu wa Mkuu wa Shule aliyehudumu kwenye shule kadhaa nchini, Godfrey Moses ilikuwa ni kuchelewa kwa baadhi ya wanafunzi kuwasili shuleni na kuanza masomo kutokana na kuchelewa kupata taarifa hizo.

"Joining Instruction zilikuwa zinapatikana shuleni na kwa mwanafunzi ambaye yuko mbali zilikuwa zinatumwa kwa njia ya posta, hivyo endapo zikichekelewa kumfikia mtoto, lazima anachelewa kufika shule kwani maandalizi yanahitajika," anasema.

Aidha anafafanua faida za kutumia njia inayotumiwa sasa ya teknolojia ya mawasiliano kuwafikishia wanafunzi, mzazi na mlezi taarifa hizo muhimu za kujiunga na shule kuwa ni uharaka ambao humwezesha mwanafunzi na familia yake kupata muda mwingi wa kujiandaa kikamilifu kwa shule.

Mwalimu huyo anasema moja ya mahitaji muhimu yanayopatikana kwenye taarifa hizo ni gharama anazotakiwa kuzilipia mwanafunzi afikapo shuleni ikiwemo karo, sare za shule na malipo mengine, taarifa za sheria za shule na fomu maalumu ya utambuzi wa afya ya mwanafunzi.

"Serikali imefanya jambo la msingi kuanza kutumia maendeleo haya ya sayansi na teknolojia kuharakisha mambo, kwa sababu wanafunzi wanahitaji muda wa maandalizi kwa ajili ya kuripoti shuleni na si ya zimamoto hasa kama matokeo ya kuchaguliwa yamechelewa kutoka," anafafanua.

Pia anasema changamoto kwenye mfumo huu inaonekana kwenye maeneo ya vijijini, ambayo hayana mtandao mzuri wa mawasiliano ya intaneti hivyo kumfanya mwanafunzi, mzazi au mlezi kushindwa kupata taarifa hizo kwa wakati sahihi.

Anasema anaamini changamoto hiyo itafanyiwa kazi na Wizara husika wakisaidiana na wataalamu wa TEHAMA ili tovuti ya wizara iwe nyepesi kiasi cha kuweza kufunguka hata kwa kutumia simu za mkononi zenye uwezo wa kupata mtandao wa intaneti.

Pamoja na hayo Mwalimu Moses anapongeza wakuu wa shule wote nchini kwa kuweza kutekeleza kwa wakati maagizo ya Waziri George Simbachawene ya kuwasilisha taarifa hizo za mwanafunzi kujiunga na shule ili zitolewe kwenye tovuti ya wizara kwa matumizi ya umma.

Kwa upande wao wanafunzi waliohojiwa na mwandishi wa makala hii juu ya mfumo huo mpya wa wizara kutoa taarifa za kujiunga na shule kwenye mtandao, wanasema ni maendeleo yanayopaswa kupongezwa huku changamoto zilizopo zikitatuliwa kwa haraka.

"Binafsi sikuamini kama naweza kupata Joining Instuction ya shule zote Tanzania kwenye tovuti ya TAMISEMI kama ilivyokuwa inatangazwa redioni, mpaka nilipoziona ndio nikajua kweli sasa Tanzania tunaendelea, ni maendeleo mazuri," anasema Philip Mhando, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dk. Didas Massaburi ya jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wazazi kwa upande wao, wanasema mwaka huu wamerahisishiwa kwa taarifa hizo za kujiunga na shule kwa mwanafunzi kupatikana kwenye mtandao kwa sababu hata kutangazwa kwa majina ya waliochaguliwa kulichelewa.

Wanasema kuchelewa huko kuliwafanya baadhi waanze kufikiria kuwapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi kwa sababu hawakujua ni lini hasa majina hayo yatatangazwa na endapo majina ya watoto wao yangekuwemo ama la.

Mmoja wa walezi anasema ni vizuri hatua hiyo ikawa endelevu na kushushwa kwenye ngazi ya elimu ya msingi, ambapo wanafunzi wa kidato cha kwanza nao watapata taarifa hizo za kujiunga na kidato cha kwanza kwa njia ya mtandao hasa wale waliochaguliwa kwenye shule za vipaji maalumu.

"Wazo langu hatua hii ishuke mpaka shule ya msingi lakini si kwa shule zile za kata ambazo mwanafunzi anachaguliwa kutoka shule moja ya msingi ndani ya kata yake kwenda shule nyingine ya sekondani ndani ya kata hiyo hiyo, nalenga zile shule za vipaji ambazo bado wanalipa ada," anasema.

Mwaka huu kwa mujibu wa Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, baada ya Wizara yake na ile ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi  kukamilisha zoezi la uchaguzi na wanafunzi kwa ajili ya kidato cha tano na vyuo vya ufundi, waliobahatika kupata nafasi hizo wanatakiwa kuwasili kwenye shule na vyuo vyao husika Julai 17, mwaka huu ili kuendelea na safari ya taaluma kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

####
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: