Monday, July 17, 2017

TADB kuunga mkono jitihada za uzalishaji Simiyu

ad300
Advertisement
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imesema itahakikisha inaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa mkoa wa Simiyu katika ubunifu wa uzalishaji wa mazao na uendelezaji wa viwanda vidogo mkoani humo.

Ahadi hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Francis Assenga, wakati alipotembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa mkoa wa Simiyu katika kikao kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka, Julai 16, mwaka huu.

Assenga alisema anatambua jitihada za uongozi wa mkoa wa Simiyu katika kubuni shughuli mbalimbali za uzalishaji mali katika mkoa huo ambazo zinalenga kunyanua hali za kimaisha za wakazi wa Simiyu hivyo .

Alisema kwa kigezo hicho, Benki yake imelenga katika kuhamasisha upatikanaji wa mikopo ya uhakika ili waweze kuchagiza jitihada hizo za wakazi wa Simiyu na kupelekea kutimiza malengo ya kimkakati ya kuanzishwa kwa Benki hiyo.

“Kila mtu anafahamu jitihada za uongozi wa mkoa wa Simiyu katika kuanzisha miradi ya uzalishaji mali mkoani humu, hivyo nasi kama taasisi ya maendeleo tuna lengo kuwapatia mikopo na kuhamasisha upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na endelevu, ili kuinua ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa kifedha nchini,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo aliongeza kuwa kupatiwa kwa mikopo hiyo nafuu kutaongeza uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo mkoani humo hali itakayochochea maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Simiyu.

Kwa mujibu wa Bw. Assenga mikopo hiyo italenga katika kuendeleza miundombinu muhimu ikiwemo ya uendelezaji waa skimu za umwagiliaji, usafirishaji, hifadhi ya mazao, usindikaji, pamoja na masoko.

“Tukiwa kama benki kiongozi  ya maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa kilimo tumelenga katika kuendeleza mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya kilimo nchini,” aliongeza.

Mapema akiwakaribisha viongozi wa Benki ya Kilimo mkaoani Simiyu, Mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka, alisema wakazi wa mkoa wa Simiyu wanahitaji msaada mkubwa wa mtaji ili kukidhi mahitaji ya sekta ya kilimo mkoani humo.

Mtaka aliongeza kuwa licha mkoa huo kongoza kwa uzalishaji wa zao la pamba ambapo Simiyu pekee inazalisha asilimia 63 ya pato lote la zao hili nchini, lakini kumekuwa na siasa kali hususan katika msimu wa ununuzi wa zao hilo.

“Tunaamini Benki ya Kilimo ikiweka mkono wake katika upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na endelevu, kutainua ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa kifedha na kutatua changamoto si tu katika zao la pamba mkoani humu bali katika sekta nzima ya kilimo Simiyu,” alisema.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: