Advertisement |
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), limetahadharisha kuwa ukosefu wa mvua kwenye ukanda wa Afrika Mashariki umeongeza njaa katika eneo hilo.
Katika taarifa yake kwa umma, FAO limesema hali hiyo imesababisha mazao mashambani kukauka, jamii kukosa lishe bora na maelfu ya mifugo kufa na kwamba wafugaji wamebeba mzigo mkubwa wa ukosefu huo wa mvua.
Tahadhari hiyo pia ilieleza kwamba mfululizo wa tatu wa ukosefu wa mvua za msimu umeathiri zaidi Somalia kusini na kati, kusini mashariki mwa Ethiopia, kaskazini na mashariki mwa Kenya, kaskazini mwa Tanzania pamoja na kaskazini mashariki na magharibi mwa Uganda.
Ilisema kwenye maeneo hayo, watu wamepoteza uwezo wao kumudu milo mitatu kwa siku huku wakiwa hawana njia mbadala za kukabiliana na baa hilo hatari kwa maisha yao.
"Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa kibinadamu katika maeneo hayo, ambayo sasa inakadiriwa kuwa milioni 16, imeongezeka kwa asilimia 30 tangu mwishoni mwa mwaka 2016," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia ilisema iwapo msaada wa haraka hautatolewa kwenye maeneo hayo, hali ya raia itakuwa mbaya zaidi kwani msimu wa kiangazi unatarajiwa katika miezi michache ijayo.
0 comments: