Friday, May 26, 2017

Jeshi la Magereza sasa kielektroniki

ad300
Advertisement
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamaji (IOM), limetoa msaada wa vifaa vya kisasa vya kielektroniki vya utunzaji kumbukumbu kwa Jeshi la Magereza hapa Nchini, vitakavyotatua changamoto mbalimbali zinazohusu utunzaji wa kumbukumbu ndani ya jeshi hilo.

Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika makao makuu ya jeshi la magereza, jijini Dar es Salaam, ambapo jumla ya seti 20 za vifaa hivyo vikiwemo kompyuta mpakato 'laptop', vinakishi 'Printer', mashine za kusoma alama za vidole na macho na vingine mbalimbali vilikabidhiwa.

Akipokea vifaa hivyo, Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Malewa, alisema vimekuja wakati mwafaka, ambapo jeshi hilo linakusudia kuhamia kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwenye uendeshaji na usimamizi wa shughuli zake za kiofisi.

Dk. Malewa alisema kutokana na changamoto ya mlundikano wa wafungwa kwenye magereza mengi nchini, utunzaji wa kumbukumbu kwa kutumia mifumo ya kizamani kwa sasa ni tatizo ambalo lilihitaji mfumbuzi wa haraka hivyo mwitiko wa IOM umefungua milango ya kumaliza tatizo hilo.

Alisema IOM limekuwa likifanya kazi kwa ukaribu na magereza, ambapo tofauti na misaada ya vifaa, shirika hilo huhakikisha linaarudisha haraka wahamaji wanaofika nchini hapa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa magereza ya hapa nchini hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi.

"Wahamaji kutoka nchi mbalimbali za kiafrika hususan Ethiopia, wamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wafungwa kwenye magereza yetu ambapo tatizo linakuwa kubwa zaidi kutokana na wao kuwa tofauti wa wafungwa wa kitanzania kwenye suala la vyakula, wengi wanachagua vyakula hivyo IOM, husaidia kuwarudisha haraka nchini mwao," alisema.

Kamishna huyo aliongeza kuwa vifaa hivyo vinatumika kukusanya taarifa za wafungwa wote wakiwemo wahamaji, ili kuwa na kanzidata (database) itakayosaidia kuwatambua wahamaji ambao awali kutokana na matumizi ya njia za kizamani, walipokuwa wakirudishwa nchini mwao kwa makubaliano ya  kutorudi, walirudi kwa majina mengine.

"Zamani tulikuwa tunatumia majina tu kuwatambua wahamaji hivyo waliporudishwa makwao waliweza kurudi tena nchini kwenda nchi za Afrika Kusini na kwingine wakitumia majina mengine kwa sababu hawana nyaraka zozote za kusafiria hivyo kwa vifaa hivi tutaweza kuwatambua kirahisi," alifafanua.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa IOM hapa nchini, Dk. Qasim Sufi, alisema wametoa msaada huo kupitia mradi wao maalumu wakishirikiana na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU), ili kufikia jamii zenye uhitaji na zinazogushwa moja kwa moja wa changamoto za wahamaji likiwemo jeshi la magereza na uhamiaji.

Alisema tangu awasili nchini, amefurahishwa na namna ambavyo jeshi hilo linakabiliana na changamoto ya wahamaji kutoka nchi mbalimbali kwa kuwatunza kwenye magereza yake likiwemo la Karanga la mkoani Kilimanjaro, ambalo alibainisha licha ya kutumia mfumo wa zamani wa kutunza kumbukumbu lina huduma nzuri.

"Tanzania iko vizuri kwenye usimamizi wa wahamaji ambao kwa sasa ni tatizo kubwa kwenye nchi nyingi; changamoto tuliyoiona hata kwenye gereza lenye huduma nzuri sana la Karanga kule Moshi ni utunzaji wa kisasa wa kumbukumbu hivyo kwa msaada huu tunaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa," alisema Dk. Sufi.

Aliongeza kuwa milango ya IOM kwa jeshi la magereza iko wazi muda wote na kwamba wataendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili ili kuhakikisha tatizo hilo la uwepo wa wahamaji haliwi mzigo kwa serikali ya Tanzania.

Hadi jana, imeelezwa kuna wahamaji takriban 800, kwenye magereza mbalimbali hapa nchini idadi ambayo ni mara nne ya iliyokuwepo Machi mwaka huu ambayo ni 298.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: