Advertisement |
Ramani kuonyesha unyeshaji wa mvua msimu wa vuli |
Tahadhari imetolewa kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi chakula na kutumia vizuri kila mvua itakayonyesha katika msimu ujao wa vuli, kwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa sehemu kubwa ya nchi kupata mvua chache kwenye msimu huo unaotarajiwa kuanza Oktoba, mwaka huu.
Kwa maana hiyo, wananchi wanaojishughulisha na kilimo wametakiwa kuandaa mapema mashamba na pembejeo ikiwa ni pamoja na kufuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa Maofisa ugani wa kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.
Pia mamlaka za maafa na wadau wengine wameshauriwa kuchukua hatua stahiki kwenye utunzaji mazingira, upatikanaji wa maji safi na usambazaji wa dawa na chakula kama hatua za awali kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza kwenye msimu huo.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kwa madhumuni ya kutangaza mwelekeo wa mvua na utabiri wa msimu wa vuli, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, alisema mvua hizo chache pia zitachelewa kuanza kunyesha maeneo mengi ya nchi tofauti na kawaida.
Alisema maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Viktoria na kusini mwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara, ndio pekee yanayotarajiwa kupata mvua za kuridhisha kwa vipindi vifupi na huku maeneo mengine yakiwa makavu kwa muda mrefu hivyo kusababisha athari kwa ustawi wa mazao ya kilimo.
Dk. Agnes alisema sababu ya mabadiliko hayo kwenye msimu wa mwaka huu wa vuli ni viashiria vilivyoko kwenye bahari kuu duniani, ikiwemo Pasifiki na Hindi, ambazo mabadiliko ya joto la bahari hizo husababisha mifumo ya hali ya hewa kubadilika.
Alisema kwa mwaka huu, vipimo vya bahari ya Pasifiki vinaonyesha uwepo wa joto la chini ya kiwango cha kawaida hivyo kusababisha hali inayojulikana kitaalamu kama ‘La Nina’ ambayo ni kinyume cha El Nino ambayo ilitokea kwenye msimu uliopita wa mvua za masika.
Alisema kitaalamu hali hiyo inasababisha bahari ya Hindi nayo kupokea mabadiliko hivyo kusababisha maeneo mengi ya nchi ya Tanzania kupata hewa kidogo ya unyevunyevu, ambao unatakiwa uwe mwingi ili kuruhusu joto kupanda angani na kusababisha mawingu ya mvua kutengenezwa.
Aidha alisema kuwa utabiri huo ambao ni wa miezi mitatu mpaka Desemba mwaka huu, unaweza kubadilika kwa baadhi ya maeneo kupata vipindi vifupi vya mvua kubwa hivyo ni wajibu wa wananchi na mamlaka zinazohusika na maafa kuchukua tahadhari kuepuka madhara.
“Maeneo mengi ya nchi tunatarajia yatakuwa makavu lakini kunaweza kuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa, ambazo zinaweza kusababisha mafuriko kwenye baadhi ya maeneo hivyo tahadhari ni vizuri zikachukuliwa na wananchi, mamlaka husika,” alisema.
Aliongeza kuwa tahadhari ichukuliwe na mamlaka zinazohusika kwa sababu kunaweza kuwa na uhaba wa malisho kwa mifugo na wanyamapori, huku pia milipuko ya magonjwa ikiwa na nafasi kubwa kutokea kwa sababu ya uhaba wa maji safi na matumizi mabaya ya mifumo ya maji taka mijini na vijijini.
Pamoja na hayo, aliyataja maeneo ya nchi na muda ambao yanatarajiwa kuanza kupata mvua za msimu akianza na kanda ya Ziwa Viktoria ambako kunapata misimu miwili ya mvua kuwa mvua zake za vuli zitaanza kunyesha kuanzia wiki ya kwanza ya Oktoba. Maeneo hayo yanajumuisha mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga.
Kwa ukanda wa Pwani ya Kaskazini, mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba na Kaskazini mwa Morogoro alisema mvua zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya tatu mpaka ya nne ya Oktoba, mwaka huu.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, alisema itapata mvua kuaznia wiki ya tatu ya Novemba huku Kanda ya Magharibi ambayo hupata msimu mmoja wa mvua ikiwemo mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa ikitarajiwa kuwa na mvua wiki ya nne ya Oktoba mwaka huu.
“Kanda ya kati, mikoa ya Singida na Dodoma huku mvua tunatarajia zitaanza kunyesha wiki ya pili ya Desemba na kiwango kitakuwa kile kile cha mvua za kiwango cha chini,” alisema Dk. Agnes.
Aliongeza: “Kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro ambako tumeiweka kwenye upande wa nyanda za juu kusini mvua zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya pili ya Oktoba mwaka huu.”
Alisema maeneo mengine yaliyosalia, mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Desemba mwaka huu kwa kiwango cha chini isipokuwa maeneo machache ya mkoa wa Mtwara.
Kutokana na utabiri huo wa TMA, baadhi ya wakulima walizungumza na Uhuru kwa simu jana, walisema hali itakuwa mbaya kwa kuwa mavuno ya msimu uliopita yalikuwa mabaya hivyo hawana hifadhi ya kutosha ya chakula.
Walisema mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaelezwa kila siku na mamlaka mbalimbali ikiwemo TMA, yameathiri shughuli zao ambazo zina changamoto ya kukosa miundombinu ya kutumia mfumo wa umwagiliaji na kwamba serikali inapaswa kuwashika mkono ili kuvuka salama kwenye msimu ujao wa kilimo.
0 comments: