Tuesday, September 6, 2016

Majambazi hatari yanaswa Dar

ad300
Advertisement

JESHI la polisi limefanikiwa kunasa mtandao hatari wa majambazi waliohusika kwenye matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha, ikiwemo uporaji wa mamilioni ya fedha kwenye benki mbili mwishoni mwa mwaka 2014, jijini Dar es Salaam.
Mtandao huo umejumuisha majambazi 10 ambao watatu kati yao wamekamatwa na jeshi la polisi ambapo baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na matukio ya wizi huo wa fedha za benki za Habib Africa na Stanbic.
Katika kuhojiwa, majambazi hao walikiri kumiliki na kuonyesha jeshi la polisi silaha walizokuwa wakizitumia kutekeleza uhalifu maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na magari mawili aina ya Toyota Noah.
Aidha walikiri kuwa ni miongoni mwa waliohusika na utekelezaji wa uvamizi wa kituo cha polisi cha Stakishari cha jijini Dar es Salaam, ambako takriban baunduki aina ya SMG ziliibwa huku askari wanne wakiuawa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kamishna wa polisi kanda maalumu, Simon Sirro, alisema majambazi hao wanaunda mtandao wa majambazi wa kimataifa ukiwahusisha raia wa Kenya ambao bado jeshi hilo linawatafuta.
Alisema mtego wa kuwanasa uliwekwa Septemba 3, mwaka huu eneo la Kawe, Keko na Mbagala kufuatia tukio la ujambazi lililofanyika Agosti 29, mwaka huu, eneo la VETA Chang'ombe, ambako walivamia ofisi ya kampuni ya Matrix na kuiba fedha.
Sirro alisema katika tukio hilo, majambazi hao wapatao 10 walikuwa wamevaa sare za jeshi la polisi na kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa kampuni hiyo huku walimwamuru Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina la Jerry Oge (28), awaonyeshe ziliko fedha za mauzo.
Alisema huku wakitishia maisha ya wafanyakazi hao kwa kufyatua risasi angani, majambazi hao waliiba kiasi cha Sh. 35,000,000 na kutoweka kwa kutumia gari lililokuwa na namba za usajili za bandia T 549 BPK aina ya Toyota Noah.
Akielezea jinsi walivyowakamata majambazi hao, Sirro alisema baada ya tukio hilo, walifanya msako mkali uliokuwa chini ya kikosi maalumu cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha ambacho kilitega mtego na kuwanasa majambazi hao watatu.
Alisema baada ya kuwakamata, pamoja na kukiri kuhusika na matukio mengine ya kijambazi, walisema Agosti 6, mwaka huu walipora bunduki aina ya Short gun yenye namba 006091830 iliyokuwa na risasi moja maeneo ya Chang'ombe viwandani wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam.
Aidha alisema upelelezi wa kina uliofanywa na jeshi la polisi kwa majambazi hao, ulibaini kuwa wanamiliki silaha nzito zikiwemo za kijeshi ambazo walizificha maeneo mbalimbali ikiwemo Mbezi chini, kwenye nyumba ambayo ilikodishwa na majambazi hao.
Kwenye upekuzi uliofanywa na jeshi la polisi kwenye nyumba hiyo, Sirro alisema kulipatikana bunduki tatu aina ya SMG zenye risasi 120 na magazine tupu nane, shortgun 3 na risasi 130, bastola 16 zilizokuwa na risasi 548 na magazine tupu moja.
Pia kulikutwa simu za sauti (radio call) 12 na chaja zake, darubini tatu, pingu za plastiki 45, vazi la kuzuia risasi (bullet proof) 3, mkasi wa kukatia vyuma vigumu, mtalimbo mmoja wa kuvunjia milango, risasi za baridi 37, boksi moja la vifaa vya kusafishia bunduki, nyundo kubwa moja na pingu tatu za chuma.
Sirro alisema vitu vingine vilivyokutwa kwenye nyumba hiyo ni mashine moja ya kuhifadhia matukio ya kamera za usalama (CCTV server), Panga moja namagari mawili aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 950 DGC na Toyota Alphard namba T 987 CLH.
"Baada ya kupata vitu hivyo, tuliwahoji zaidi watuhumiwa hao na wakatuambia kuna silaha zingine wamezificha kwenye msitu wa Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambako tulienda," alisema Sirro.
Alisema walipofika msitu wa Vikindu majira ya usiku ambako ni eneo lililodaiwa na watuhumiwa hao kuwa ndiko walipoficha silaha hizo, walipokelewa na milio ya risasi iliyorindima kutoka wanakokwenda hivyo kuwalazimu askari kulala chini.
Sirro alisema wakiwa bado wamelala chini, zilisikika sauti zikisema "MMETUUA SISI" huku risasi zikiendelea kufyatuliwa hovyo na majambazi wengine waliokuwa eneo hilo.
Alisema majambazi watatu waliokuwa wamekamatwa awali, ambao pia waliambatana na polisi ili kuonyesha eneo hilo, walichelewa kulala chini hivyo walipigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na kufa kabla hawajafikishwa hospitali kwa matibabu.
"Baada ya risasi mfululizo, majambazi tulioambatana nao walichelewa kulala chini hivyo walikuwa wamejeruhiwa vibaya kifuani na tumboni jambo lililosababisha wavuje damu nyingi sana na walifariki wakiwa kwenye gari la polisi wakiwa njiani kwenda hospitali," alisema.
Alisema kwenye msitu huo, askari walikamata bunduki nyingine aina ya SMG iliyokuwa imetelekezwa na majambazi hivyo kufanya idadi ya bunduki za aina hiyo kufikia nne kutokana na msako huo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema kikosi maalumu cha jeshi la polisi cha kuzuia wizi wa magari kimewakamata watu wanne kwa makosa ya wizi wa magari nane yalioibwa na kuuzwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Saalam na mikoa ya jirani.
Alisema magari yaliyoibwa na watu hao ni Toyota Carina namba T 838 BHH, Toyota Noah T 206 DEC, Toyota Spacio T 874 DFG, Toyota Spacio T 668 DDG, Toyota Spacio CD 380, Toyota namba T 783 BCW, Toyota Probox T 490 BWP na Mitsubishi Fuso namba T 588 DDE.
Alisema kati ya magari hayo, Toyota Spacio CD 380 lilikuwa likimilikiwa na Mwanadiplomasia wa Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini.
Aidha kupitia oparesheni zinazoendela kufanywa na jeshi hilo, Kamanda Sirro alisema Septemba 29, mwaka huu, Kinondoni jijini Dar es Salaam, watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kuvunja nyumba na kuiba nyakati za usiku walikamatwa.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Seleman Mohammed (24), Twenye Abdallah (35), James Emmanuel (35), Bimu Yahaya (26) na Abdallah Mohammed (25) na Deogratius Oscar (19) wote wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema upelelezi wa matukio hayo unaendelea ambapo watuhumiwa waliohusika kwenye uhalifu huo wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo.  
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: