Advertisement |
Mvua hiyo iliyoambatana na radi ilianza usiku wa kuamkia jana na kuendelea mpaka mchana wa jana hali iliyo yaacha maeneo mengi ya jiji yakiwa hayapitiki na mengine kupitika kwa shida kutokana na mitaro ya maji ya mvua kuzidiwa nguvu.
Akizungumza na Uhuru jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mvua hizo ni za kawaida kwenye msimu na kwamba zitaendelea kunyesha kwenye baadhi ya maeneo ya mkoani Dar es Salaam hadi kesho.
Gazeti la Uhuru lilifanya ziara kwenye baadhi ya maeneo yakiwemo TAZARA, Buguruni, baadhi ya sehemu katikati ya jiji, Kigogo na Jangwani na kushuhudia watu wengi wakitembea kwa miguu huku wakiwa wameshikilia viatu mkononi kukwepa kuvilowesha na maji.
Kutokana na hali hiyo malalamiko mengi ya wakazi hao wa jiji yalielekezwa kwa halmashauri husika kutokana na uzembe uliopo katika kuhakikisha mitaro yote muhimu inazibuliwa kila mara ili kuepuka kutuama kwa maji ambayo yanaleta usumbufu kwao.
Walisema mitaro mingi ya jiji haihimili mvua hata ya kiasi kidogo na kwamba endapo zitanyesha mvua kubwa za El nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), miundombinu mbalimbali inaweza kuharibiwa kwa kiasi kikubwa na kuisababishia serikali hasara kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema hawajui ni lini mamlaka husika zitatekeleza wajibu wao wa kukomesha adha inayowapata wananchi wa Dar es Salaam wakati wa vipindi vya mvua.
“Hatujui hii shida itaisha lini, tumeona kawaida tu sasa kuwa kila mtu ukiona mvua ujue ukitoka nyumbani jiandae kuvua viatu na kutembea peku ukifika sehemu kutokana na kutuama kwa maji njiani,” alisema mmoja wa wakazi hao.Aidha alisema ni aibu kwa uongozi wa jiji pale ambapo kunanyesha mvua ndogo lakini madhara yanakuwa makubwa kutokana na kukosekana kwa njia sahihi, madhubuti za kudhibiti maji ambayo kwa kawaida yakikosa sehemu ya kwenda hutuama na kuleta usumbufu mkubwa magari na watembea kwa miguu.
Samson Mushy, ambaye ni Mwanafunzi wa chuo cha maji kilichoko Ubungo, naye alisema maji yana desturi ya kuwa na nguvu kama zilivyo nishati zingine hivyo endapo mamlaka husika zitaendelea kupuuzia uwepo wa miundombinu mibovu ya maji barabarani madhara yatakuwa zaidi zaidi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mvua.
Naye Mkese Patrick, ambaye ni Daktari kutoka moja ya hospitali jijini, alisema maji yaliyotuama na madhara makubwa kwa jamii kiafya na kwamba jamii haitakiwi kukubali uwepo wa maji ya aina hiyo katika mazingira yao.
“Ni kweli asubuhi hii nimeona maeneo mengi maji yametuama, si jambo zuri kiafya kwa jamii kwani madhara yake ni makubwa. Kuna aina nyingi za magonjwa yanayosababishwa na uwepo wa maji yaliyotuama kwenye mazingira yetu.
“Kunatakiwa kuchukuliwe hatua za haraka ili miundombinu ya maji isiwe na kizuizi jambo litakalosababisha maji yakija yapite yote kwa kuwa hatupaswi kuyaruhusu yasimame, huu ndio ushauri wa kitaalamu,” alisema Daktari huyo.Kunyesha kwa mvua hiyo jijini Dar es Salaam ni baada ya kupita wiki takriban tano bila kuwepo kwa mvua katika maeneo mengi ya mkoa huo huku joto likiongezeka maradufu jambo linalounga mkono utabiri wa TMA kwa msimu wa vuli, ambao ulisema kutakuwa na upungufu wa mvua kwa kiasi kikubwa katika mkoa huo.
Utabiri wa TMA wa saa 24 hadi kufikia jana mchana ulionyesha uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani kwenye maeneo mengi ya nchi hususan maeneo ya mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa ya nyanda za juu kusini na kusini magharibi.
0 comments: