Friday, March 6, 2015

Wabunge Dar wachachamaa

ad300
Advertisement

WABUNGE wa Dar es Salaam wametaka Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA) na Jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT)  kukutana ili kuangalia namna ambavyo wataweza kufanya mashine za  EFD kuwa rafiki kwa wafanyabiashara.
Baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam

Pia wamesema kutokana na changamoto nyingi ambazo zinawakabili wafanyabiashara, watahakikisha mwaka huu viongozi wake wanaingia bungeni ili kuwasilisha hoja zao. 
Hata hivyo, walisema JWT inatakiwa itambuliwe kisheria na bunge kutokana na kwamba ndio wachangiaji wakubwa wa uchumi wa nchi.
Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, alisema hayo jana wakati wa mkutano uliofanyika jana na Jumuia ya Wanyabiashara Tanzania.
Mtemvu alisema kutokana na changamoto nyingi ambazo wafanyabiashara hao wanapitia wanatakiwa kuwa na msemaji wao bungeni.
Alisema pia anashangazwa na jambo ambalo lilitakiwa kuunda kamati ya  uchunguzi wa EFD ambalo halijafanyika hadi sasa na kwamba hajajua sababu zake.
Mtemvu alisema atahakikisha  kamati hiyo inaundwa kwa sababu hakuna sababu yoyote ya msingi inayozuia kufanyika hivyo.
Pia alisema watendaji wa sekta mbalimbali waache tabia ya kuwarushia mzigo wabunge hata mambo ambayo hayawahusu, jambo ambalo limekuwa la kawaida.

"Mimi niseme tu kila mtu atende kazi kulingana na idara yake, imekuwa kawaida kwa watendaji kufanyia wananchi ukatili halafu wakiulizwa wanasema hilo ni agizo la wabunge. Huo ni uongo.

Zipo sheria ambazo kama bunge tunazipitisha lakini kwa sasa imezuka tabia ya kuzijazia mafuta na kuonekana kwa mwonekano mwingine," alisema.
Naye Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu, alisema kutokana na wafanyabiashara kusema hawana mpango wa kuacha kulipa kodi ila mfumo ulipo ni kandamizi, wiki ijayo watakutana kuangalia namna ambavyo wataweza kuirekebisha.
Zungu alisema kuhusiana na upandishwa wa kodi kwa asilimia 100,  watatoa agizo kwa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Biashara, kukutana na wafanyabiashara kulizungumzia hilo.
Alisema anachotaka Kariakoo itambuliwe kama ni Ukanda wa Uchumi wa nchi, hivyo kwa kushiriakiana na Wabunge wenzake, watahakikisha  kamati ya uchunguzi inaundwa.
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alisema wafanyabishara wamechelewa kuwashirikisha  katika shughuli zao na badala yake wanawashirikisha wakati ambapo wameshindwa kabisa.
Alisema pamoja kwamba wamechelewa lakini watahakikisha kuwa baadhi ya sheria zinafanyiwa marekebisho kwa lengo la kutatua baadhi ya kero zao.
Pia alisema kabla hawajaanza bunge lazima baadhi ya matatizo ya wafanyabishara hao yanatatuliwa kwakuangalia kamati mojawapo bungeni na kuja kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo hapa Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema kama hayatapatiwa ufumbuzi kupitia kamati hiyo Mbunge mmojawapo atateuliwa kwenda kuwasilisha changamoto za wafanyabisha Bungeni.

"Kutokana na wafanyabishara wenyewe kusema kuwa hawatambui chombo chochote kinachowatetea, Jumuiya hii inatakiwa kutambulika rasmi Bunge kama taasisi yao,"alisema.

Sambamba na hilo Mnyika alisema matokeo ya serikali kukosa mapato ya fedha yasipelekee kuwabana wananchi hasa katika suala la Jeshi la zimamoto.
Alisema fedha ambazo wafanyabishara wamekuwa wakizitoa kama huduma ya zimamoto zimekuwa zikitumika kama posho ya watendaji badala ya kuongeza vitendea kazi kama magari ya zimamoto.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Philimin Chonde, alisema lengo kubwa la kukutana na wabunge hao ni kuwafikishia matatizo makubwa ambayo wamekuwa wakikumbana nayo.
Mwenyekiti huyo alisema wamekuwa wakikumbana na matatizo mengi lakini kubwa zaidi ni suala la upandishwa wa kodi holela na kwamba hadi sasa imepandishwa kwa asilimia 100.
Pamoja na hilo alisema suala la leseni ni kizungumkuti kutokana na ukweli kwamba wamekuwa wakilipia lakini wanapewa risiti baada ya mwaka mmoja.
Chonde alisema mfumo wa ulipiaji wa leseni si mzuri,  hivyo wanaiomba serikali kuangalia utaratibu mwingine wa kuuweka kama ambavyo stika za magari zinalipiwa kila baada ya mwaka ili kuwaepushia usumbufu.
Katibu wa Jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdalla Mwinyi, alisema wanahitaji kulinda mitaji yao hasa wakati huu ambapo kodi inapandishwa holela.
Alisema mfumo wa ulipaji kodi si rafiki kwao japokuwa wanapenda kulipa kodi kwaajili ya maendeleo ya nchi lakini sasa imefika wakati mgumu ambapo ulipaji wa kodi umepanda na kufikia asilimia mia.
Mwinyi alisema pia wanahitaji uwazi bandarini kwani kumekuwepo na tozo ambazo zinaendelea bila yao wao kunufaika na biashara husika kwa maana ya tozo ambazo sio halali.
Hata hivyo alisema kuwa mashine za EFD zinawasaidia TRA kujua mapato lakini kwa wafanyabishara zinasababisha mitaji yao kufa kama hazitafanyiwa marekebisho.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: