Sunday, February 1, 2015

Utalii utaubeba uchumi - Mkapa

ad300
Advertisement


RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amesema ana imani na sekta ya utalii nchini kuwa ni suluhisho la kudumu kwenye maendeleo endelevu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuliko sekta nyingine.

Amesema imani hiyo inatokana na idadi kubwa ya sekta binafsi nchini, zinazoweza kushirikiana na serikali katika jitihada za kuijengea uwezo sekta hiyo kwa gharama yoyote huku wakitanguliza kwanza maslahi ya taifa.

Mkapa aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi, kwenye mkutano wa sita wa kujadili hali ya uchumi, ulioandaliwa na Benki ya Dunia na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema licha ya kuwa na uelewa hafifu wa masuala ya utalii, ni mtaalamu wa uchumi, ambaye muda wote aliokuwa madarakani kwenye nyadhifa tofauti serikalini, aliamini kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa sekta ya utalii kuwa hawaoni matumaini kama inavyoelezwa kinadharia. Ninaiamini serikali, inafanya kazi na sekta binafsi kwa kiasi kikubwa na mimi siku zote ninajua pande hizi zikishirikiana hakuna kinachoharibika,” alisema Mkapa.

Aliongeza kusema kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo mengine ya nchi, hasa nyanda za juu kusini, kwa sababu kwa muda mrefu vivutio vya kaskazini na visiwa vya Zanzibar ndiyo vimepewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia hapa nchini, miaka kumi kuanzia sasa sekta ya utalii itawezeshwa katika maeneo yote, ikiwemo kuboresha miundombinu na itasaidia ongezeko la pato la taifa kwa takribani sh. bilioni 16.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwenye mkutano huo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Phillip Dongier, alisema sekta ya utalii ndiyo pekee inayoweza kuitoa Tanzania mahali ilipo sasa kiuchumi kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya kipekee.

Alisema baadhi ya mambo ambayo yanakwamisha sekta ya utalii nchini kuzalisha kama inavyotarajiwa na wengi ni pamoja na ushirikishi mdogo wa jamii kuhusu uhifadhi, mifumo mibovu ya kuendesha shughuli za utalii, ikiwemo kulipia gharama za utalii kwa njia ya mtandao na tozo kubwa la kodi.

Dongier alisema mapungufu hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka na wizara husika na wadau wengine wa utalii, zikiwemo sekta binafsi ambapo serikali kwa kiasi kikubwa inatakiwa kuhakikisha inasimamia suala la kupungua kwa kodi kwenye masuala yanayohusu utalii.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema serikali imeshaanza kufanya jitihada za kuifanya sekta ya utalii kuwa tegemeo kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kufungua utalii nyanda za juu kusini mwa Tanzania, kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alisema pia kuwa wameendelea na mapambano dhidi ya ujangili kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na kutafuta usuluhishi kati ya Tanzania na Kenya kwenye masuala ya utalii, ambayo siku chache zilizopita kulikuwa na kutokuelewana baina ya pande hizo.

Alisisitiza kuwa kamwe hakutakuwa na vita ya kibiashiara kwenye sekta ya utalii kati ya Kenya na Tanzania, kwani wanafanya mazungumzo ya amani ya kutafuta suluhisho na kamwe Tanzania haipendezwi wala kunufaika na matatizo ya kiusalama yanayoikumba Kenya kwa sasa.

Nyalandu alisema sekta ya utalii nchini licha ya kuandamwa na changamoto kadhaa, imeendelea kufanya vizuri katika kuongeza fedha za kigeni, ambapo mwishoni mwa mwaka uliopita kulipokuwa na hofu ya ugaidi kutoka nchi jirani ya Kenya na maambukizi ya virusi vya ebola, bado idadi ya watalii haikushuka chini ya kiwango.

“Tulikuwa na hofu juu ya hali ya utalii itakavyokuwa nchini kwenye miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliopita kutokana na hali ya usalama ilivyokuwa kwa wenzetu jirani (Kenya) na maambukizi ya ebola barani Afrika, lakini hali ilikuwa nzuri sana kwa sababu wageni bado waliendelea kuingia nchini kwa wingi,” alisema Waziri Nyalandu.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: