Sunday, February 1, 2015

CWT: Tunamwamini Anna Kilango

ad300
Advertisement

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema muda muafaka umefika kwa matatizo lukuki yanayowakabili walimu nchini kwa muda mrefu, kutatuliwa ipasavyo kutokana na maboresho yaliyofanywa na Rais ndani ya wizara husika siku chache zilizopita.

Maboresho hayo yamehusisha mabadiliko ya nafasi ya Naibu waziri katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambapo Rais Dk. Jakaya Kikwete, alimbadilisha Jenista Muhagama aliyekuwa kwenye nafasi hiyo na kumteua Anna Kilango.


Akizungumza na blog hii kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa CWT, Yahya Msulwa, alisema licha ya kuwa mbunge wa kawaida kwa kipindi kilichopita, Anna Kilango amekuwa mtetezi wao kwa muda mrefu ndani ya bunge kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu walimu.


Alisema ni mmoja kati ya mihimili waliyokuwa wakiitegemea kwa kipindi kirefu hasa inapofika nafasi ya kutoa hoja zinazoihusu wizara ya elimu na ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo kwa sasa imepewa pia dhamana na kushughulika na masuala ya elimu kwa ngazi ya msingi na sekondari.


Msulwa alisema matatizo ya walimu yanajulikana na Mama Kilango, lakini watafanya utaratibu wa kumtembelea Naibu Waziri huyo ofisini kwake, kwa lengo la kumkabidhi rasmi jukumu la kupambana nayo kwa kushirikiana na Waziri Dk. Shukuru Kawambwa, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha 2014/2015.


Pia alisema CWT imeridhishwa na hatua ya serikali ya kusimamia kidete kukamilika kwa ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari nchini, ambapo kwa shule ambazo hazikukamilisha baada ya Desemba 9 mwaka jana, zimetakiwa kukabidhi majengo hayo serikalini Mei mwaka huu.


Alisisitiza kuwa kutokana na hatua hiyo, ajira za walimu wa masomo ya sayansi zitolewe kwa wingi, ufanisi na kwa wakati ili waweze kutoa mchango chanya wa maendeleo ya wanafunzi kitaaluma kupitia masomo ya sayansi, ambayo kwa muda mrefu yameonekana kuwa tatizo kutokana na kukosekana kwa vitendeakazi na walimu wakutosha.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: