Friday, September 1, 2017

Mbivu, mbichi za Agosti 8, kujulikana leo Kenya

ad300
Advertisement
Waswahili wanasema mbio za sakafuni huishia ukingoni.

Ndivyo inavyotabiriwa kuwa kwenye kesi inayohusisha chama cha Jubilee na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC), dhidi ya muungano wa NASA kwenye kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa tano wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Upande wowote utakaodondokea pua kwenye kesi hiyo, ni wazi mbio zake ndo zitakuwa zimefikia mwisho au ukingoni wa 'Saga' hilo la kuifukuzia ikulu ya Kenya haswa. 

Wakati hayo yakisubiriwa kwa hamu na watu wengi hususan wa ukanda wa Afrika mashariki baadaye leo Septemba 1, wabunge na maseneta waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu, jana walianza kula kiapo.

Shughuli za uapishaji huo zilifanyika jana katika majengo ya bunge la nchi hiyo, jijini Nairobi kutekeleza agizo la Rais Mteule, Uhuru Kenyatta aliyetaka bunge la 12 liendelee na kazi zake kama kawaida.
 
Jumla ya wabunge 290 kutoka maeneo bunge yote yaliyoko nchini humo mbali na walioteuliwa kuwakilisha vyama vyao, walianza kuapishwa jana asubuhi kwenye shughuli iliyotabiriwa ya kuchukua takriban saa 17.
 
Kwa upande wa Maseneta wa Kaunti 47 waliochaguliwa na kuteuliwa kuwakilisha vyama vyao walimaliza kula kiapo katika bunge la seneti lililoko katika Ukumbi wa KICC, jijini Nairobi.
 
Baada ya kiapo chao, viongozi hao walitakiwa kumchagua spika wa bunge la kitaifa na yule wa bunge la seneti.
 
Muungano wa National Super Alliance (NASA), awali ulisema wabunge wake wasingehudhuria hafl a hiyo katika kile kichoonekana kuwa ni kutaka kupuuza wito wa Rais Uhuru Kenyatta kuliagiza bunge liendelee na shughuli zake.

NASA, walidai kuwa Rais Kenyatta hana mamlaka ya kuagiza bunge liendelee na kazi, hadi pale mahakama ya juu ya nchi hiyo itakapotoa uamuzi wa kesi inayoendelea kupinga ushindi wa kiongozi huo.
 
Hata hivyo Jumatano wiki hii, NASA ililegeza msimamo wake na kuwaruhusu wabunge wake kuhudhuria hafla hiyo ya kula kiapo.

“Tumekubaliana kwa kauli moja kuwa wabunge wetu ambao ni zaidi ya 100 wahudhurie kikao cha kwanza bungeni,” alisema Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alipohutubia kikao cha waandishi wa habari Lavington, Nairobi kwa niaba ya NASA.

Wetang’ula ambaye pia ni kinara mwenza wa NASA na kiongozi wa chama chake cha Ford Kenya, aliongeza: “Ajenda inayowalazimu kuhudhuria ni kuapishwa pekee wala hakuna biashara nyingine.”
 
Seneta huyo aliyeweza kutetea kiti chake alidokeza kuwa muungano wa NASA utaandaa mkutano wa wabunge wake wiki ijayo ili kujadili utendakazi wao.
 
“Wiki ijayo tutakuwa na kamati ya wabunge wa NASA ili kuzungumza kuhusu utendakazi wetu,” alisema.
 
NASA ilipinga ushindi wa Rais Kenyatta ambaye alipata asilimia 54 ya kura zilizopigwa huku kinara wa NASA, Raila Odinga akipata asilimia 44 pekee.
 
Kipingamizi chao kilisimamia hoja kuwa uchaguzi huo haukuwa halali, wakiinyooshea kidole Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa imehusika kwenye uchakachuaji wa matokeo.

Madai hayo yamepingwa vikali na mawakili wa IEBC tangu siku ya kwanza ya shauri hilo la kihistoria tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini humo.

Shauri la Raila kupitia NASA, lilianza kusikilizwa Jumanne wiki hii na majaji saba wa mahakama ya juu ya Kenya, ambapo uamuzi rasmi utatolewa leo.
 
Haja ya Raila kwenye kesi hiyo ni kuitaka mahakama hiyo ifute matokeo yote ya urais na kuagiza kufanyike uchaguzi mwingine kwa nafasi ya urais pekee.

Endapo mahakama itatupilia mbali kesi hiyo NASA, Rais Kenyatta ataapishwa siku 30 baada ya uamuzi wao na kama itaamua uchaguzi wa kiti cha urais haukuwa wa huru, haki na wazi basi uchaguzi mwingine utaitishwa baada ya siku 60 kutoka siku ya maamuzi hayo.

Rais Kenyatta wa Jubilee na Tume ya IEBC inayoongozwa na Mwenyekiti wake Wafula Chebukati ndio washtakiwa wakuu kwenye kesi hiyo.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: