Advertisement |
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa polisi wa mkoa wa kipolisi wa Temeke, Kihenya wa Kihenya, alisema tukio la kwanza la Mwanamke kujinyonga lilitokea juzi, Kongowe kanisani saa 12 jioni.
Alisema upelelezi wa awali ulionyesha Mwanamke huyo, Hamisa Mohamed (24), alichukua uamuzi huo baada ya kukalishwa chini na familia yake kutokana na kubadilisha dini ndani ya ndoa bila idhini ya mume wake.
Kamanda huyo alieleza kuwa kwa mujibu wa Mume wa marehemu, Ibrahim Twalib (36), Hamisa alikuwa ni muumini wa dini ya kiislamu kabla ya Januari mwaka huu alipoamua kuhamia kanisa la Christian Life lililoko Kongowe.
Alibainisha kuwa hatua ya Mwanamke huyo kubadilisha dini haikuridhiwa na mume wake, ambaye alifanya kila jitihada kumzuia bila mafanikio ndipo alipoamua kutoa taarifa kwa wazazi wa mke wake.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, ilielezwa kuwa marehemu aliendelea na tabia hiyo ambapo juzi hali ilikuwa mbaya baada ya kuamua kubatizwa katika kanisa hilo na kuitwa jina jipya la Joyce Mohamed.
Kamanda Kihenya alisema hatua hiyo iliwalazimu wazazi wa mwanamke huyo kufika nyumbani kwao na ili kumkanya juu ya uamuzi huo, ambapo mara baada ya kikao hicho alijifungia chumbani kwake na kujinyonga kwa kutumia mtandio.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Temeke huku upelelezi zaidi juu ya tukio hilo ukiendelea.
Wakati huo huo Kamanda Kihenya wa Kihenya, alisema tukio lingine lililotea siku hiyo hiyo saa 4 asubuhi eneo la Bamba Mwongozo-Kigamboni, ambapo fundi umeme Michael Gabriel (47), alikufa baada ya kuanguka kwenye nguzo ya umeme.
Alisema fundi huyo mwajiriwa wa kampuni ya ujenzi ya Salem ya jijini Dar es Salaam, alianguka kutoka kwenye nguzo ya umeme licha ya kujifunga mkanda wa usalama na kupata majeraha makubwa sehemu za kichwani.
Kwa mujibu wa Kamanda Kihenya, Fundi huyo alipoteza maisha katika hospitali ya Vijibweni alikopelekwa kupatiwa matibabu. Mwili wake umehifadhiwa kwenye hospitali hiyo wakati jeshi la polisi likiendelea na upelelezi.
0 comments: