Advertisement |
Wametakiwa kuhakikisha kunakuwepo idara moja itakayofanya kazi za Wizara hiyo kwa uharaka na ufanisi tofauti na idara tatu zilizopo hivi sasa.
Wito huo ulitolewa jana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa, wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika Makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA).
Waziri alisema idara tatu zilizopo kwenye Wizara hiyo, idara ya Mawasiliano, idara ya Tehama na kitengo cha Tehama kwa maoni yake hazina umuhimu wa kuwepo kama wana nia ya kupata maendeleo katika ulimwengu huu wa Sayansi na teknolojia.
Alisema angependa kuona inabaki idara moja kati ya hizo ambayo itakuwa ikisimamia vitengo vidogo vinavyofanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya Nchi kwenye nyanja ya teknolojia ulimwenguni.
Pia aliwataka Wafanyakazi hao kutoogopa kuachia madaraka waliyonayo sasa endapo idara hizo zitaunganishwa kwakua ili maendeleo yawepo lazima kukubali mabadiliko.
Mbarawa alisema kuunganisha idara hizo kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za serikali, muda na matumizi mengine ya rasilimali za serikali zinazopotea sasa kwa ajili ya ukubwa wa ofisi.
Kwa upande wa uchapakazi wa Wizara kwa kipindi cha nyuma, aliwapongeza kwa kusema kuwa kazi imefanyika kwakua kwa miaka kumi iliyopita Wizara imefanya mambo makubwa ikiwemo kuboresha mkongo wa taifa wa mawasiliano.
Alisema Wizara yake inaendelea na kazi ya kuutawanya mkongo huo kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa biashara Nchini kutokana na kukosekana mawasiliano, ambapo hadi kufikia Juni 2015, Serikali itakuwa imetumia Sh. milioni 93 kwa usambazaji huo.
0 comments: