Advertisement |
WATANZANIA waishio Geneva nchini Uswisi kupitia chama chao cha TAS, wametoa msaada kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani Orphanage Centre kilichopo mkoani Dar es Salaam ikiwa ni njia mojawapo ya kusaidia malezi ya watoto hao wanaohitaji msaada wa serikali na jamii kwa ujumla ili kufikia malengo yao ya Maisha.
Msaada huo wa vifaa ambavyo ni pamoja na tangi la kuhifadhia maji, samani za kusomea, jiko na mtungi wa Gesi uliwasilishwa kituoni hapo jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi kwa niaba ya wanachama hao waliopo nchini Uswisi.
Wakati wa uwasilishaji huo, Dk Kijazi alielezea upendo walionao watanzania hao kwa kuwakumbuka watoto wa kituo cha Amani.
"Upendo huu ni mfano wa kuigwa kwa watanzania waishio ndani na nje ya nchi. Inafurahisha sana kuona ndugu zetu waliopo nje ya nchi (Diaspora), wanakumbuka nyumbani kwa kuwasaidia wahitaji, basi hii iwe changamoto kwa wote," alisema Dk. Kijazi.
Pia aliwahakikishia watoto wa kituo hicho kwamba TAS na TMA wanawapenda na kila mara wamejitahidi kuwakumbuka mara fursa inapopatikana, ambapo mpaka sasa wanawake wa TMA wameshasaidia kituo hicho kwa kipindi kilichopita.
Akipokea msaada huo msimamizi na mwanzilishi wa kituo cha Amani Bi. Margareth Mwegalawa aliwashukuru TAS kwa kuwakumbuka watoto wa Amani hata kuwawezesha kupata vifaa hivyo muhimu, na alimuomba Dk. Kijazi kuwasilisha salamu hizo kwa kusisitiza msaada huo ni mkubwa kulingana na uhitaji wake.
Aidha akizungumza kwa niaba ya watoto wenzie, mtoto Beatrice Phine alisema wamefurahi kwa kupata vifaa hivyo vitakavyoboresha maisha yao na mazingira ya kusomea na kumuomba Dk. Kijazi awafikishie salaam zao za upendo na shukrani kwa TAS.
Chama hicho cha watanzania waishio Uswisi kimekuwa kikitoa misaada kwa wahitaji nchini ambapo mwanzoni mwa mwaka huu walitoa Sh.500,000 kwa Mama Aida wa mkoani Mbeya aliyejifungua watoto wanne.
Msaada uliwasilishwa kwa niaba ya TAS na meneja wa TMA kanda ya nyanda za juu kusini magharibi, Issa Hamad.
0 comments: