Tuesday, February 25, 2014

Ukweli kuhusu Afya ILALA..

ad300
Advertisement
AFYA ni moja kati ya mambo muhimu sana ya kuzingatia katika maisha ya mwanadamu. Hakuna ujanja katika hili!

Tofauti na masuala mengine, afya ndio muhimili wa utendaji kazi wa mtu yeyote kwani humuwezesha mwanadamu kufanya shughuli yoyote kwa ufanisi.

Mtu akiwa na tatizo lolote kiafya huwa hawezi kuwa kama ilivyokuwa kawaida kumuona kuanzia kitabia mpaka muonekano wa nje.Ni wazi kuwa ananyong'onyea na wengine huwa hawapendi kabisa kuonekana na wengine mara awapo mgonjwa.

Si kwa binadamu tu, bali hata kwa viumbe hai wengine ugonjwa unapowaingia wanakuwa tofauti na hulka yao.

Na kwa kawaida suluhisho la ugonjwa ni kupata tiba inayolingana na ugonjwa husika, popote ama kwenye tiba za miti shamba au dawa zilizotayarishwa kitaalamu zinazopatikana kwenye maeneo maalum ikiwemo vituo vya afya.

Hivyo ni bayana kuwa utoaji wa tiba unatakiwa ufanywe kwa ufanisi wa hali ya juu ili mtu aweze kupona kutoka kwenye ugonjwa unaomsumbua, kwani matibabu hafifu ni sawa na kupalilia tatizo.

Kote nchini vituo vya kutoa huduma za afya vimesambaa ili kuhakikisha huduma hiyo inamfikia kila mtu katika eneo husika, lakini vituo hivyo vinaelemewa na wingi wa watu wanaopatikana kwenye maeneo hayo.

Serikali zetu, zinajukumu kubwa la kuhakikisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi wake zinafanikiwa lakini tatizo linakuja pale ambapo kunatengwa fungu la fedha za kununua dawa na vifaa vya vituo vya kutolea afya kulingana na idadi ya watu inayopatikana kwenye eneo hilo.

Tatizo hilo halikwepeki, kutokana na hali halisi iliyopo kuwa kila kitu kinafanyika kutokana na takwimu zilizopo.
Ninamaanisha nini? Serikali inahaja ya kujua idadi ya wananchi wake kila baada ya muda fulani, ili tu iweze kutoa huduma kulingana na uhitaji wa watu hao isizidishe wala kupunguza.

Ni zoezi muhimu kiuchumi lakini lina matatizo makubwa, kwani kuna maeneo yanayotoa huduma kwa jamii ambayo yanakuwa yanapewa mahitaji na Serikali kuu kulingana na makisio ya idadi ya watu inayolizunguka eneo hilo, huku idadi hiyo ikiwa mara tatu mpaka nne kwani watu wengine wanatoka maeneo ya mbali kufuata huduma mbalimbali kwenye maeneo mengine kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ubora wa huduma husika .  

Kwa mfano ulio hai kabisa ni hali ilivyo kwenye manispaa kubwa nchini kama Ilala.

"ZAIDI ya wakinamama 100 wanajifungua kwenye hospitali ya Amana kwa siku. Hizi ni takwimu tulizonazo kwa sasa, takwimu ambazo si mpya sana lakini hali ndio iko hivyo".

Hiyo ni idadi kubwa kulingana na hadhi ya hospitali tunayoiongelea, idadi ambayo kwa mikoani ni idadi inayobebwa na hospitali kubwa ya mkoa au rufani".

Hayo ni baadhi tu ya yaliyoelezwa na kaimu mganga mkuu wa Manispaa hiyo ya Ilala, kuhusu hali ya utoaji wa huduma za afya kwenye eneo lao la huduma.

Ilala ni moja ya Manispaa za mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ndio Manispaa iliyopo katikati ya jiji hilo ambalo ni kitovu cha biashara nchini.

Wingi wa watu kwenye Manispaa hii ni kubwa hivyo huduma za afya pia zinatakiwa kuwa za kutosha ili ziweze kuwahudumia watu wengi waliopo.

Kutokana na umuhimu wake kibiashara, watu wanatoka kando ya mji kufuata huduma katikati ya jiji ambapo ndipo mahali ilipo Manispaa hii.

Ukitaja sehemu mbili tu za Kariakoo na Posta lazima kengele ya hatari italia kwenye kichwa cha mtu kwa kumaanisha ni sehemu ambazo zina sifa ya kipekee, uwingi wa watu ikiwa ni miongoni mwa sifa hizo.

Kwa maana hiyo, kutokana na kuwepo kwa Hospitali 1 kubwa, Vituo vya afya viwili na jumla ya Zahanati 23 kwenye manispaa ya Ilala kama eneo hili lingekuwa linahudumia  wakazi wake tu, huduma za afya zisingekuwa na matatizo kabisa.

Lakini hali haipo hivyo, kwa mujibu wa Kaimu mganga mkuu wa manispaa hiyo, Dk. Willy Sangu, amesema asilimia zaidi ya 50 ya wagonjwa wanaohudumiwa na vituo vyao vya afya sio wakazi wa Manispaa ya Ilala bali ni wale wanaotoka ama Kinondoni au Temeke.

Alieleza kuwa hali hiyo inawapa changamoto za kiutendaji kadri siku zinaposogea kwani Serikali inawaajiri watumishi wahudumie vituo vya afya vya Eneo hilo kulingana na idadi ya vituo hivyo na idadi ya watu wa eneo hilo.

Hivyo wale wanaoongezeka kutoka maeneo mengine, wanakuwa ziada ya bajeti iliyopangwa na Serikali kwa maana kuwa mahitaji yanazidi uwezo wa watoa huduma waliopo kwenye Manispaa hiyo.

Ni changamoto! Kwani huwezi kumzuia mtu asihudumiwe kwenye vituo vya afya vya Ilala kisa tu yeye ni mkazi wa manispaa ya Temeke au Kinondoni, huwezi.

Daktari Sangu alisema wagonjwa hao wana mahitaji yao kulingana na ugonjwa walionao, kwa mfano wajawazito wanahitaji pamba, mipira ya kuvaa mikononi, maji pamoja na dawa. Vyote hivi vinakuwa vimepangiwa bajeti kwa ajili ya watu waliopo Ilala!

Kwahiyo Serikali ikilitambua hili, itahakikisha inatoa fedha za ziada kuwasaidia watu wanaoongezeka kwenye vituo vya kutoa huduma za afya kutoka mbali na maeneo ya huduma yaliyokuwa yamekisiwa na serikali yahudumiwe na kituo husika. 

Tena ihakikishe inaweka wasimamizi wanaotambua wajibu wao kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na ufanisi wa hali ya juu, ili sehemu zote ziwe na huduma bora na watu wasikimbie maeneo yao kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kufuata huduma bora ambazo hazitolewi na vituo vyao vya afya.

Kwa Ilala, Mwenyezi Mungu anawapigania kwani mazingira ya kazi yanawabana sana watu wa afya kutokana na hali halisi iliyopo ya kukinzana kwa mahitaji ya watu na kitu kilichopo.

Ni sawa na baba wa familia ya watoto watano ambaye amenunua vipande viwili vya mkate akidhamiria awape watoto wake mara afikapo nyumbani na kila mmoja apate sawa sawa. Ni kitu kisichowezekana, sana sana watagawana lakini hawatatosheka.

Serikali imeonyesha nia ya dhati kutimiza wajibu wake kwenye sekta ya afya kwakuruhusu mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na afya, kama vile AMREF, Medical development of Health (MDH) na Pathfinder, kuingia kwenye maeneo mbalimbali nchini na kutoa misaada ya afya kifedha, vifaa, dawa na hata wafanyakazi.

Hilo limeonekana suluhisho kwa kiasi fulani, kwani hospitali nyingi nchini zimenufaika na zinaendelea kunufaika na misaada hiyo kwa kuboresha huduma za afya zikiwemo hospitali za Manispaa ya Ilala.

Kaimu mganga mkuu wa Manispaa ya Ilala, alitoa wazo la kujenga kwa jamii ya Watanzania kwa ujumla. Wazo ambalo mimi ninaliunga mkono bila shaka yoyote, kwani alisema kila Mwananchi afanye jitihada za kuwa na bima ya afya ama ya serikali au hata zile binafsi.

Alisema kiafya itamsaidia mtu huyo kwani atakuwa na uhakika wa kupata huduma muda wowote, mahali popote bila hata kuwa na fedha taslimu za matibabu.

"Bima inamnufaisha mwananchi na sisi watoa huduma za afya kwani kwa upande wetu mtu akija na bima anakuwa kama ametuletea hundi,"

Na yeye kwa kumjali, hospitali zote za Manispaa yetu tumeboresha huduma za bima kwa kutenga vyumba maalum vya kuona wagonjwa, vifaa na matabibu waliobobea kwa ajili ya watu wenye bima tu," alisema daktari Sangu.

Sasa, mimi ninaona japo sekta ya afya inaandamwa na changamoto kadhaa ni wajibu wa kila Mwananchi kuzingatia taratibu za afya kwa kujitunza kiafya katika nyanja zote za afya.

Ufuatiliaji wa masuala ya afya ni muhimu, kwani itamsaidia mtu kutambua umuhimu wa kuwahi hospitalini mara aonapo mabadiliko yoyote kiafya katika mwili wake na kuacha kuona ni hali ya kawaida, na kusema aah...... hii Itapita!

Na serikali nayo, kwa nafasi yake ibebe jukumu la kuajiri watumishi wengi lakini wenye vigezo. Sio wale wanaomfanyia upasuaji wa mguu mtu mwenye uhitaji wa upasuaji wa kichwa na kumfanyia upasuaji wa kichwa kumfanyia upasuaji wa Mguu.

Pia kutoa vifaa vya kutosha kwenye hospitali zote zinazohitaji vifaa vya kutosha kulingana na uhitaji na hadhi ya Hospitali husika.

Ninaamini kwa kufanya hivyo, mambo yatakuwa mazuri katika sekta ya Afya tofauti na ilivyo sasa, hivyo ninaitakia Serikali kila la kheri katika juhudi zake za kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi muhimu kwenye bara la Afrika inayompatia kila Mwananchi maisha bora ikianzia na Afya.  
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: