Friday, February 28, 2014

Wafanyakazi wa Reli Tanzania watishia kugoma.

ad300
Advertisement
WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Reli Tanzania kupitia chama chao (TRAWU), wametishia kufanya mgomo iwapo Serikali haitawaongezea kima cha chini cha mshahara kama ilivyotangaza mwezi Julai mwaka jana.

Kama moja ya taasisi za serikali, walitarajia kupandishiwa kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 41 kuanzia julai mwaka uliopita.

Katika kikao kilichofanyika jana kwenye viwanja vya shirika la reli mjini Dar es Salaam, wafanyakazi hao ambao ni wanachama wa TRAWU walitishia kutoendelea na kazi kwa kudai wako kwenye kikao ambacho kitaahirishwa mpaka Serikali itakapotimiza maombi yao.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa TRAWU kanda ya Dar es Salaam, Shehe Shughuli alisema wafanyakazi wa reli wananyanyaswa na serikali kwa kupewa kiasi cha sh. 205,000 kwa mwezi, ambacho kwa maisha ya sasa hakitoshi.

Alisema kikao hicho wamekiandaa kama muendelezo wa kikao kilichofanyika Februari 6, mwaka huu ambapo walikutana na Mkurugenzi wa TRAWU aliyepewa mapendekezo ya kuwasiliana na Wizara juu ya malalamiko yao.

Mwenyekiti huyo alisema mapendekezo yao ni kuongezewa sh. 95,000 kwenye mshahara wanaoupata sasa kama nyongeza ya asilimia 41 iliyoahidiwa na serikali kwa wafanyakazi wa taasisi zote za serikali.

Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kaimu mkurugenzi wao, ombi lao lilifikishwa serikalini na kuahidiwa kuongezwa mshahara lakini hawajatimiziwa ndipo walipofikia uamuzi wa kuishurutisha tena serikali kwa kikao cha jana.

Akizungumza katika kikao hicho, Gwamaka Mwakangole ambaye ni mfanyakazi wa reli kitengo cha mawasiliano alisema wamechoka kukandamizwa, na umefika wakati wa kupata haki yao kama wafanyakazi wengine wa serikali.

"Matatizo yalianzia TRC ilipobinafsishwa, mpaka leo TRL tunaumizwa kisa eti hatuzalishi. Sababu ya reli kutozalisha chanzo kikubwa ni Serikali yenyewe sio sisi, sisi TRAWU tunakaa kimya mpaka kieleweke," alisema Gwamaka.

Hata hivyo katika kulitatua hilo, Wizara ya Uchukuzi ilituma barua kuwataka viongozi wa TRAWU kukutana na waziri wa Uchukuzi ofisini kwake jumatatu ijayo, jambo ambalo wanachama walilipinga mpaka alipofika Mkurugenzi wa TRL, Kipallo Kisamfu kuwaasa warudi kazini wakisubiri utekelezwaji wa maombi yao.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: