Advertisement |
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limesema kuwa, ukata unaolikabili shirikisho hilo ndiyo unaokwamisha kuanza kwa kambi ya timu ya taifa ya riadha.
Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema kambi hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya michuano ijayo ya Jumuia ya Madola.
Kinyang'anyiro hicho ambacho kimepangwa kuanza Julai 23, mwaka huu mjini Glasgow, Scotland, Tanzania inatatarajiwa kuwakilishwa na timu za michezo mbalimbali ikiwemo ile ya riadha.
Nyambui alisema awali shirikisho lake lilipanga kuwa kambi kwa kikosi hicho, ambacho alisema kinatarajiwa kuundwa na wanariadha 40 ianze Desema Mosi, mwaka jana kule mkoani Dodoma.
Alisema lakini baada ya kuibuka janga la ukosefu wa fedha kwenye RT, alisema hatimaye walijikuta wakishindwa kuanza kambi kama walivyopanga.
"Kwa kweli tunapenda sana kuiweka timu yetu kambini kwa muda mrefu, kwa ajili ya maandalizi kabla ya kushiriki michuano ijayo ya Jumuia ya Madola. Lakini tatizo la ukata linatukwamisha," alisema.
Katibu huyo alisema mpango mkakati wa awali wa RT unaonyesha kuwa kinahitajika kitita cha shilingi milioni 400, ili kuwaweka kambini wachezaji hao.
Akifafanua zaidi, alisema kambi hiyo ambayo imepangwa kuwa ya muda mrefu ina lengo la kujenga kikosi bora, ambacho alisema kitakuwa kikiiwakilisha Tanzania kwenye michunao mbalimbali ya kimataifa.
"Napenda wadau wafahamu kuwa kambi hii haina maana tu kwa ajili ya kucheza michezo ya Madola, ila ina lengo pia la kuwa na kikosi bora ambacho kinaweza kuiwakilisha nchi kwenye michuano mingine ya kimataifa mfano ile ya Olimpiki," alisema.
Alisema uongozi wa shirikisho lake unaendelea kujipanga vyema, alisema ili kuhakikisha kuwa lengo la kupata kiasi hicho cha fedha linafanikiwa.
0 comments: