Advertisement |
SERIKALI
imepokea mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa megawati 75 kwa ajili ya
mradi wa Kinyerezi I ambao unatarajiwa kukamilika Oktoba, mwaka huu.
Mitambo
hiyo kutoka Marekani, ilipokewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ambaye alikuwa ameambatana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi
Felchesmi Mramba, katika bandari ya Dar es Salaam.
Maswi
alisema mradi wa Kinyerezi I utazalisha megawati 150 na kwamba mitambo
hiyo ni ya awamu ya kwanza ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati
75.
"Serikali tunatekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi katika kupunguza ghrama za uzalishaji umeme. Meli hii kubwa ina shehena ya mitambo ya kuzalisha megawati 75 ambayo tutaisimika Februari 28, mwaka huu," alisema.
Alisema
mitambo hiyo haitakuwa na athari kwa kuwa ni ya kisasa na awamu ya pili
itawasili nchini mwezi ujao. Mitambo hiyo imetengenezwa na kampuni ya
General Electric.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Mramba, alisema kuwasili kwa
mitambo hiyo ni hatua za msingi za kutatua tatizo la umeme nchini,
ambapo tangu uhuru uwekezaji wake ulikuwa duni.
"Katika historia ya nchi tangu Uhuru hatujawahi kuwa na uwekezaji mkubwa kama huu. Mitambo ya kuzalisha umeme itatatua suala la uzalishaji umeme hivyo bado usafirishaji na usambazaji. Watanzania tuna mipango mingi inayotekelezeka jitihada za leo (jana) ni sehemu ya mipango hiyo," alisema.
Mhandisi
Mramba alisema katika eneo la Kinyerezi kuna miradi minne ambayo ni
Kinyerezi I, II, III, IV ambayo itapunguza matatizo ya uzalishaji umeme.
Aliwaomba
Watanzania kuwa na subira kwa kuwa matatizo ya umeme yatafika mwisho
kutokana na miradi mikubwa iliyopo ambayo utekelezaji wake ni wa makini
na madhubuti.
Kwa
upande wake, Meneja wa Miradi ya Uzalishaji Umeme TANESCO, Mhandisi
Simon Jirima, alisema mitambo hiyo itahifadhiwa katika eneo la mradi na
baada ya uzalishaji, umeme utaingizwa kwenye gridi ya taifa.
Mhandisi Jirima alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 183 (zaidi ya sh. bilioni 250).
0 comments: