Advertisement |
Wanataaluma katika
fani mbalimbali hapa nchini wametakiwa kutojivunia usomi na maarifa waliyopata
na badala yake wafanye kazi ili kusaidia jamii inayowazunguka kuondokana na
changamoto mbalimbali.
Hayo yalisemwa
na Mwanazuoni wa Kiswahili, Profesa Tigiti Sengo (pichani aliyesimama), wakati wa hafla ya kukumbuka
uzoefu na mchango wake katika taaluma na hususani katika lugha ya Kiswahili iliyofanyika
katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dar es Salaam.
Katika hafla
hiyo iliyohudhuriwa na wadau wa lugha kutoka ndani na nje ya Tanzania, Profesa
Sengo alisema wakati umefika kwa wasomi mbalimbali kufanya tafiti zitakazotoa
majibu ya changamoto mbalimbali katika Jamii badala ya kujisifu.
“Kuna umuhimu wa
wasomi na watafiti kufanya tafiti katika masuala mbalimbali kama dini na dhana
zake ili kuisaidia Jamii badala ya kuacha watu wakipotoka,” alisema.
Pia alisema ni
muhimu kwa jamii kufahamu kuwa changamoto ni sehemu ya maisha hivyo kutafuta
majawabu na kujenga mazingira ya kutetea haki bila woga.
Kwa upande wake,
Profesa Abdala Safari, ambaye ni mwandishi wa vitabu alisema maisha ya Profesa
Sengo ni mfano wa kuigwa na wasomi wa Tanzania kwa kuwa ametumia muda mwingi
kujibu changamoto mbalimbali za Jamii kwa kuwasaidia kupata mahitaji yao.
“Wasomi wana
wajibu mkubwa wa kutumia muda wao kusaidia jamii kwa kutoa ushauri ili Jamii
itekeleze yatakayosaidia kuinua Jamii husika kimaendeleo,” alisema Profesa
Safari.
Aidha aliwataka
wasomi kuandika vitabu na matini mbalimbali vitakavyosaidia Jamii kupata
maarifa na ujuzi kama mbinu ya kumuenzi Profesa Sengo.
Said Masomaso, Mhadhiri katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania alisema kuwa Profesa Sengo ametoa mchango mkubwa
katika kutafsiri maneno mbalimbali ya kisayansi na teknolojia katika lugha ya
Kiswahili.
“Naishauri
serikali kuendelea kuwasaidia wazee kama hawa kwani wana mchango mkubwa katika
Jamii,” alisema Said.
Profesa Tigiti
Sengo ni mhadhiri mwandamizi ambaye amewahi kuhudumu katika vyuo vikuu
mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi na ameandika zaidi ya vitabu sitini,
machapisho na matini zadi ya 100 katika lugha ya Kiswahili ambayo yanasaidia
jamii kupata maarifa katika mada mbalimbali za lugha, fasihi, na sarufi.
Imeandikwa na Vincent Mpepo, OUT
0 comments: