Advertisement |
Shirika la Umoja wa Mataifa la
Mpango wa Chakula Duniani (WFP), limelazimika kupunguza mgao wa chakula
kinachotolewa kwa wakimbizi 320,000 wanaoishi katika kambi za Mtendeli, Nduta
na Nyarugusu mkoani Kigoma kaskazini magharibi mwa Tanzania kwa sababu ya upungufu
wa fedha.
Imeelezwa kuwa chanzo ni uhitaji wa haraka
wa jumla ya Dola za Marekani milioni 23.6, kuanzia sasa hadi Desemba mwaka huu,
ili WFP imudu kuendelea kutoa mgao unaokidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa
wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania.
Akizungumza mkoani Kigoma jana,
Michael Dunford ambaye ni Mwakilishi wa WFP hapa nchini, alisema shirika lao hugawa
vyakula vya aina tano tofauti kwa wakimbizi ambao kimsingi wanatoka Burundi na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema vyakula hivyo ni pamoja na
unga wa mahindi, kunde, Nafaka Kuu, mafuta ya mbogamboga na chumvi na kwamba kwa
sababu ya upungufu wa fedha, aina zote tano za vyakula kwa Agosti zimekidhi
asilimia 62 ya kiasi cha kalori 2,100 zinazopendekezwa kitaalamu kutosha
mahitaji ya mtu ya siku.
“Pasipo mwitikio wa haraka kutoka wa
wahisani, itakuwa lazima kupunguza mgao kwani akiba ya chakula inapungua kwa
kasi sana,” alisema Mwakilishi wa Nchi wa WFP Tanzania Michael Dunford.
Pia aliongeza: “Wakati ambapo WFP
inashukuru sana kwa msaada uliokwishatolewa hadi sasa, tunatoa wito ili
wahisani waitikie haraka na kuwasaidia wakimbizi na kutoa fedha zaidi ili
tugawe mgao kamili na kuzuia athari mbaya zisidumu kwa muda mrefu.”
Alisema kupunguza mgao kunasababisha
matatizo mengi yanayoweza kubadili vibaya maisha ya wakimbizi. Kupunguza kiasi
cha kalori na msaada wa lishe kunaweza kusababisha utapiamlo mkali na kuongeza
uwezekano wa kupata magonjwa.
Licha ya aina hizo tano za vyakula,
Shirika la WFP pia hugawa vyakula vya moto kwa wakimbizi mara baada ya
kuwasili, mgao wa chakula cha nyongeza kwa wanawake wajawazito na wanawake
wanaonyonyesha na msaada wa chakula kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini na kwa
watu wanaoishi na VVU/UKIMWI.
Hadi sasa vyakula vya moto vinavyogawiwa
kwa wakimbizi wanaoingia nchini na programu ya chakula cha nyongeza
havijaathiriwa na punguzo la sasa la mgao.
0 comments: