Wednesday, August 30, 2017

TMA, BAKITA kushirikiana

ad300
Advertisement







Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema imeanza mazungumzo na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ili kutafuta tafsiri rahisi ya maneno ya kitaalamu yanayotumiwa kwenye utabiri wa msimu na ule wa kila siku wa hali ya hewa.

Imesema  hatua hiyo itasaidia wananchi wengi kuelewa kwa haraka utabiri husika ambao kwa nyakati tofauti umehusisha maneno ya kisayansi yasiyo rahisi kuelewekewa na jamii yote hasa watu wa hali ya chini.

Akizungumza leo Agosti 30 jijini Dar es Salaam,  kwenye warsha ya wanahabari ya kujadili msimu ujao wa Vuli, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema kwa kupitia vyombo vya habari, TMA inaendelea kujizatiti kutekeleza majukumu yake ipasavyo. 

Mkurugenzi huyo amesema moja ya malengo yao ambayo watakuwa wanayaendeleza kwa kuyaboresha ni kuwafikia wananchi wengi zaidi katika lugha nyepesi inayoeleweka kutokana na umuhimu wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii. 

Amesema hiyo ndiyo sababu kuu ya kuamua kuanzisha ushirikiano na BAKITA ili taarifa husika ambazo kiuhalisia  zina mchango mkubwa kwenye kuandaa mipango ya maendeleo na utekelezaji wake katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ujenzi wa miundombinu na afya zifanye kazi inayotakiwa. 

"Nafurahi kuwajulisha kwamba tayari Mamlaka imekwisha wasiliana na BAKITA na wamekubali tuwasilishe maneno hayo ili yajadiliwe na kupatiwa tafsiri rahisi itakayoeleweka kwa watumiaji na sisi tutayaleta kwenu wanahabari," amesema.

Kuhusu utabiri uliopita wa msimu wa masika 2017,  Dk. Kijazi alivishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri za kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa usahihi hali iliyosababisha wapate mrejesho wa mara kwa mara kutoka maeneo mbalimbali. 

Alisema utabiri huo ambao uhakika wake ulikuwa asilimia 87.5 ulisaidia kuhakikisha taarifa zilizoboreshwa na kukidhi mahitaji ya watumiaji kufika kunakotakiwa na kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na athari zinazotokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Katika msimu wa mvua za masika uliopita kuanzia Machi hadi Mei mwaka huu maeneo mengi ya nchi yetu ilipata mvua za chini ya wastani kama ilivyokuwa imeainishwa katika utabiri huo mvua hizi hazikuwa na mtawanyiko mzuri.

"Hali hii ilisababisha kuwepo kwa kipindi hicho hivyo kupelekea ukanda wa mvua kutoimarika katika maeneo mengi ya nchi  mzuri," amesema Dk. Kijazi.

Hata hivyo, amesema kwa maeneo ya ukanda wa Pwani hususan mkoa wa Tanga, kulitokea vipindi vya mvua kubwa mwezi wa April 2017, vilivyosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya Lushoto ambapo kwa upande wa visiwa vya Unguja na Pemba ilisababisha mafuriko, vifo na uharibifu wa mali.

Alitumia fursa hiyo kuahidi kutangaza utabiri wa msimu wa vuli unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba na kufika mwisho Desemba, ifikapo Septemba 4, mwaka huu. 

Wanahabari waliohudhuria warsha hiyo walisema wamejifunza mengi yatakayowasaidia kuboresha namna yao ya kuripoti habari za hali ya hewa kwa jamii. 




Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: