Advertisement |
Wanufaika 121 wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF katika kijiji cha Kilindi, kilichopo kata ya
Matiri wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma wamejiunga na mfuko wa bima ya afya.
Akizungumza na Blog hii ofisini kwake leo Agosti 29, Ofisa Mtendaji wa
kijiji hicho, Maula Komba, alisema wanufaika hao baada ya kuhamasishwa juu
ya umuhimu wa kujiunga na mfuko huo kwa pamoja waliridhia kutekeleza hilo.
Walisema sehemu ya fedha zao waliamua kulipia bima hiyo hali ambayo imekuwa
msaada mkubwa kwao pindi wanapougua na kulazimika kwenda katika zahanati, kituo
cha afya au hospitali.
Maula alisema kabla ya uamuzi
huo wa kujiunga na bima ya afya wanufaika wa mpango huo wa kunusuru kaya
masikini walikuwa wakikosa uwezo wa kulipia huduma za matibabu jambo ambalo
wakati mwingine lilikuwa likipelekea baadhi yao hata kupoteza maisha.
Baadhi ya wanufaika hao wakiwemo Osiana Kapinga na Imelda
Milinga, waliipongeza serikali kwa kutekeleza vizuri mpango huo wa kunusuru kaya
masikini hivyo kusababisha jamii hiyo iondokane na matatizo makubwa
waliyokuwa wakikumbana nayo kwa muda mrefu ikiwemo kuwa na uhakika wa kupata
huduma bora za matibabu pindi wanapougua.
Joyce Ngatunga na Augeni Hyera
nao walisema kitendo cha wao kuhamasishwa kujiunga na bima ya afya kutawafanya
waweze kuendelea na kazi za uzalishaji mali kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli
kwamba sasa wanauhakika wa kupata matibabu bure kwa kipindi kirefu.
"Sasa fedha tunazozipata badala ya kuzielekeza kwenye huduma za matibabu zitakuwa na
kazi moja tu ya kusaidia katika mapambano dhidi ya umasikini wa kipato kupitia
kilimo na shughuli zingine za kiuchumi," alisema Joyce.
Walisema wamekuwa wakinufaika
na mpango huo tangu awamu ya kwanza ambapo fedha walizozipata waliamua kuanza
kufuga kuku ambao kwa sasa wamefikia 60 kutoka kuku kumi waliowanunua awali.
0 comments: