Advertisement |
Wizara ya Nishati na Madini imetoa mafunzo ya Mfumo wa pamoja wa
Kukusanya Maduhuli ya Serikali (GePG) kwa Maafisa Madini na Wahasibu wa
Wizara hiyo ili kuboresha shughuli za ukusanyaji maduhuli.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhasibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Anthony Tarimo alisema kuwa mafunzo yamelenga
kuwawezesha washiriki kuuelewa vyema mfumo huo ili kuwa na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali wenye tija.
Tarimo alisema serikali imeamua kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli kuwa
wa kielektroniki ili kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli na vilevile
kuongeza uwazi miongoni mwa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
“Kupitia mfumo huu, Serikali inao uwezo wa kujua maduhuli yote yanayoingia kwa wakati mmoja kwa sababu umeunganishwa na Wizara na Taasisi mbalimbali,” alisema Tarimo.
Aidha alibainisha kuwa Mfumo huo wa
GePG ulianza kutumika rasmi Julai, 2017 na kwamba kwa upande wa Wizara
ya Nishati na Madini mafunzo ya awali yalitolewa kwa watumishi wa Ofisi
ya Madini- Kanda ya Mashariki ambayo inahusisha ofisi za madini za Dar
es Salaam, Pwani, Tanga, Handeni na Morogoro.
Alisema Mfumo huo ni
rafiki na kwamba utaboresha na kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli na
kwamba mara baada ya mafunzo, washiriki watakuwa na uwezo wa kuutumia
ipasavyo.
Tarimo alisema mafunzo hayo yanawahusu Wahasibu, Maafisa
Leseni pamoja na watumishi wengine ambao kwa njia moja ama nyingine
wanahusika na utoaji wa hati za madai za malipo mbalimbali.
Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanahusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali
kutoka kwa wataalam wa TEHAMA wa Wizara ya Fedha na Mipango na wa
Wizara ya Nishati na Madini na pia yatahusisha majadiliano ili kuboresha
utendaji kazi wa watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli.
“Wanasheria pia watawasilisha mada ili kuelewa vyema mabadiliko katika
Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika hivi karibuni,” alisema
Tarimo.
Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyikia katika Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA) kuanzia leo Agosti 28, 2017 kwa
kushirikisha zaidi ya washiriki 100.
0 comments: