Advertisement |
Kutokana na umuhimu wake, uvuvi umepewa sifa ya kuwa sekta rasmi ambayo mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi unatambuliwa na bajeti kuu ya serikali ya kila mwaka.
Licha ya hilo, unapozungumzia Tanzania ya Viwamda, huwezi kuacha kuitaja sekta ya uvuvi kama moja ya mzalishaji mkubwa wa malighafi za viwanda hususan vile vya nyama na usindikaji kwa ujumla.
Sekta hii kwa mujibu wa wataalamu akiwemo Reuben Shempemba, ambaye ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya sayansi ya majini na uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inatoa kiasi kikubwa cha ajira, kipato, kujipatia riziki, fedha za kigeni na mapato kwa Taifa.
Anasema hana uhakika na takwimu za hivi karibuni kwenye suala zima la ajira zinazotokana na uvuvi, lakini ni moja ya sekta chache ikiwemo Kilimo na Madini ambazo zinatoa fursa nyingi za ajira rasmi na zisizo rasmi kwenye ukanda wote wa Pwani ya Tanzania na Kanda ya Ziwa.
Shaka ya Reuben kwenye takwimu za sasa inaondolewa na taarifa ya tovuti rasmi ya wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi inayosema sekta ya uvuvi inaajiri zaidi ya watu 4,000,000 wanaojishughulisha na uvuvi na shughuli zinazohusiana na uvuvi, wakati zaidi ya waendesha uvuvi 400,000 wameajiriwa moja kwa moja kwenye sekta hii.
Kwa upande wao, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, inasema Mwaka 2016, sekta ya uvuvi ilikua kwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 2.5 ya mwaka 2015.
Aidha, ulaji wa mazao ya uvuvi kwa mtu kwa mwaka ni kilo 8.0 ikilinganishwa na kilo 16.7 zinazopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO, 2011).
Inasema Mwaka 2016, jumla ya tani 362,595 za samaki zilivunwa ikilinganishwa na tani 362,645 zilizovunwa mwaka 2015 ambapo kati ya kiasi kilichovunwa, tani 308,629 zilitoka maji baridi na tani 53,823 kutoka maji chumvi ikilinganishwa na tani 309,922 zilizovunwa kutoka maji baridi na tani 52,723 kutoka maji chumvi mwaka 2015.
"Mwaka 2016, mazao ya uvuvi tani 39,691.46 na idadi ya samaki hai wa mapambo 65,841 iliuzwa nje ya nchi na kuiingizia Serikali mapato ya sh. bilioni 14.3 ikilinganishwa na mazao ya uvuvi tani 40,540.95 na idadi ya samaki hai wa mapambo 42,100 iliyouzwa nje ya nchi na kuiingizia Serikali kiasi cha sh. bilioni 12.9 mwaka 2015," inasema taarifa hiyo ya NBS kwa mwaka 2016.
Aidha, licha ya mafanikio hayo na mchango wa sekta ya uvuvi kwenye maendeleo inaelewa kuwa kuna changamoto kubwa kutoka kwa wananchi wenyewe wanaotumia nguvu na akili zao zote kuharibu rasilimali hizo kutoka baharini kwa manufaa yao na ubinafsi.
Ili kupunguza uharamia huo kwenye mazao ya uvuvi, serikali ilipanga kufanya doria ambayo kwa mwaka 2016, jumla ya doria zenye siku kazi 4,328 zilifanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikilinganishwa na doria zenye siku kazi 5,985 zilizofanyika mwaka 2015.
Taarifa rasmi ya NBS inasema katika doria hizo, zana haramu zikiwemo nyavu kokoro 968, kamba za kokoro zenye urefu wa mita 742,356, nyavu za makila 3,096 zenye macho madogo; nyavu za dagaa 483 na nyavu za utali 15,753 zilikamatwa.
Nyingine ni vyandarua 33 vya mbu, nyavu za kimia 32, katuli 16, mikuki 3,408, mabomu 17, V6 explosive vipande 600, Detonator vipande 35, tambi za baruti 2, mbolea ya urea kilo 252, mitungi ya gesi ya kuzamia 55, mitumbwi 338, injini za mitumbwi mitano.
Watuhumiwa mbali na kukamatwa na zana hizo haramu kwa uvuvi inaelezwa walikutwa na samaki wachanga aina ya Sangara kilo 14,015, sato kilo 39, kaa kilo 50, kambakoche kilo 172, nyama kilo 16, majongoo bahari kilo 48, magamba ya starfish kilo 12, dodoji (seahorse) vipande 775, makome ya baharini kilo 401 mapezi, mataya ya papa kilo 14.5 na matumbawe kilo 75.
Jumla ya watuhumiwa waliokamatwa ni 293 ambapo kesi 21 ziliwasilishwa mahakamani na sh. milioni 37.7 zilikusanywa kama faini na kuiongezea serikali mapato na kujizatiti zaidi kwenye kukomesha matukio hayo kwa kutoa elimu ya usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi kwa wavuvi 10,000 kupitia maonesho ya nanenane (Dodoma), siku ya chakula Duniani (Arusha) na siku ya uvuvi duniani (Kigoma).
Mbali na mafunzo hayo, wavuvi na wadau wa uvuvi 631 kutoka Halmashauri za Mkuranga (93), Temeke (130), Bagamoyo (288), Kinondoni (130) na maofisa wa uvuvi wilaya kutoka wilaya 16 za ukanda wa Pwani walipatiwa mafunzo ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa kuzingatia mfumo wa ikolojia na mazingira.
Changamoto hiyo ya uvuvi haramu licha ya kuonekana kuwa kubwa zaidi mtaalamu kutoka Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), anasema magugu maji ndio tatizo kubwa zaidi kwa usalama wa samaki hasa ziwani.
Mtaalamu huyo, Mashindano Lawrance, anasema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, waliamua kutengeneza mashine ya kisasa ya kuvuna magugu kutoka majini na kuyasaga kwa ajili ya kuzalisha mbolea za kilimo.
Anasema mashine hiyo imeundwa kwa umbo mithili ya boti, ambapo kazi yake kubwa ni kuangamiza mimea yote ya majini jamii ya magugu ambayo huharibu mazalia ya samaki na kupunguza idadi ya samaki majini kwa kukatisha maisha yao kabla hawajakomaa na kuzaliana.
"Magugu yanazuia uzalishaji wa samaki, kwa sababu hujifunga funga kwenye maeneo ya mazalio na kusababisha ikolojia kuvurugika," anasema.
Anasema magugu ni hatari zaidi kwa kuwa yanasambaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa maana kwamba yana uwezo wa kuziba eneo kubwa la maji na kufanya hewa ya oksijeni isiwafikie samaki na hivyo kusababisha vifo vya samaki.
Mwisho, ni wazi hakuna asiyefahamu kwamba Tanzania imejaaliwa kuwa na maliasili nyingi za majini kwa kuwa na jumla ya eneo la maji la bara takriban kilomita za mraba 61,500 au kiasi cha 6.5% ya jumla ya eneo la ardhi.
Eneo hilo la maji ni kilomita za mraba 62,000 linalogawanyika kwa mgawanyiko kuwa kilomita za mraba 35,088 ni ziwa Viktoria, kilomita za mraba 13,489 ni ziwa Tanganyika, kilomita za mraba 5,760 ni ziwa Nyasa, kilomita za mraba 3,000 ni ziwa Rukwa, kilomita za mraba 1,000 ni Ziwa Eyasi na kilomita za mraba1,000 ni maeneo mengine ya maji.
Maeneo mengi haya ya maji tafiti zinasema yana samaki wengi bila kuizungumzia bahari ambayo kwa upande wake, nchi ina bahari ya kilomita za mraba 64,000 na ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1,424.
Ukanda Maalumu wa Kiuchumi (EEZ) unafika maili za baharini 200 katika eneo la kilomita za mraba 223,000 na kuipa nchi eneo la bahari la nyongeza na maliasili za uvuvi, hivyo wananchi hawana budi kushirikiana na serikali na mamlaka zingine kutunza utajiri huu kwa kila hali kwa maslahi ya taifa.
0 comments: