Advertisement |
Shamba la miti la Sao Hill kwa kushirikiana na Kampuni ya Art International limeanza
utafiti wa kugema utomvu wa miti ya msindano kama njia ya kujiongezea kipato.
Akizungumza
na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mabadiliko ya tabia nchi ya nchini Malawi,
iliyotembelea Shamba hilo hivi karibuni, Meneja wa Sao Hill, Salehe Beleko, alisema ushirikiano huo ni kwa lengo la kuongeza pato la shamba hilo.
"Katika kuongeza vyanzo vya mapato tumeingia mkataba na kampuni hii kufanya
utafiti na ikibainika kwamba haitaathiri ukuaji wala ubora wa miti
tutakuwa tumepata chanzo kipya cha mapato," alisema.
Alifafanua
zaidi kuwa wanatarajia kuuza kila kilo moja ya utomvu kwa sh. 750 hivyo
endapo kutakuwa na uzalishaji mkubwa shambani humo, utakuwa utajiri
mkubwa kwa miaka ijayo kutokana na uhitaji wake sokoni.
Meneja huyo alisema kwa kuanzia utafiti wamelenga miti iliyokuwa tayari kuvunwa
na kama wakiona hakuna madhara wataendelea kwenye miti michache yenye umri mdogo.
Alisema
matokeo
ya utafiti huo yatasababisha kuwepo kwa ama ruhusa rasmi ya kukuza miti
hiyo kwa ajili ya kuvuna malighafi hizo ama kukataza kabisa zoezi hilo.
Naye
mtaalamu wa kampuni ya Art kutoka China, Yhoung Zhoung, alisema taasisi yake imefuata taratibu zote za
ugemaji na usafirishaji wa utomvu huo.
Alisema
kwamba kampuni yake
inahitaji miti millioni mbili kwa mwaka ili kupata ujazo wa utomvu
wanaouhitaji na kwamba watafurahi kama Sao Hill litakuwa moja ya eneo la
kupata malighafi hizo.
Akijibu
swali la mke wa Rais wa zamani wa Malawi, Patricia Muluzi ambaye pia ni
mjumbe
wa kamati hiyo, aliyetaka kujua matumizi ya utomvu huo, Yhoung alisema
baada ya kuchakatwa na kuchanganywa na kemikali mbalimbali hutumika
kutengenezea dawa mbalimbali, bazoka (chewing gum) na gel.
Mjumbe
mwingine wa Kamati hiyo kutoka Malawi, Rashid Msusa, alisema kwa mara ya kwanza wameshuhudia
matumizi mapya ya zao la mti, teknolojia ambayo hawajawahi kuiona nchini
kwao Malawi.
Kamati
hiyo mara baada ya kumaliza ziara hiyo Sao Hill, waliahidi kufuatilia
matokeo ya utafiti huo ili kama utakuwa chanya, ikiwezekana wauhamishie
Malawi ambako kuna miti ya jamii mbalimbali.
0 comments: