Advertisement |
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) vimekubaliana kuanzisha Shahada ya Uzamili katika elimu ambayo itawalenga wahitimu wa shahada ya kwanza wanaotarajiwa kuwa walimu katika vyuo vya mafunzo ya ufundi hapa nchini.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana kati ya uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kuhudhuriwa na viongozi wa pande zote mbili.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda, alisema kumekuwa na walimu wanaofundisha vyuo vya ufundi hapa nchini lakini hawana maarifa katika masuala mbalimbali ya saikolojia na mbinu za ufundishaji hivyo ushirikiano huo utasaidia kuandaa wakufunzi wenye sifa stahiki.
“Makubaliano kati ya OUT na VETA yanahusisha kufundisha nadharia kwa njia ya masafa na mafunzo ya elimu kwa vitendo ili kuwa na wahitimu wanaokidhi sifa na ubora”, alisema Profesa Bisanda.
Aliongeza kuwa kumekuwa na walimu wa elimu ya ufundi hususan waliosomea masuala ya uhandisi katika ngazi ya shahada ambao hawana mafunzo yoyote na sifa stahiki ya kuwa walimu hivyo kozi hii itasaidia kupata wakufunzi wenye sifa ya ualimu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha VETA Morogoro, Anamringi Maro, alisema ushirikiano kati ya VETA na OUT utasaidia kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu kwani utawaongezea ujuzi wakufunzi wa vyuo vya ufundi katika masuala ya ufundishaji.
“Vyuo vingi vinavyosimamiwa na VETA na kuto aelimu ya ufundi hapa nchi havina walimu wenye sifa hivyo tukaona tutumie fursa hii kushirikiana na OUT katika kuanzisha shahada ya uzamili ili kurekebisha hali hiyo”,alisema Bwana Maro.
Naye Mhadhiri na Mratibu wa programu hiyo, Profesa Elinami Swai, alisema mafunzo hayo ni fursa kubwa kwa nchi kwani imekutanisha utambuzi wa elimu rasmi na isyo rasmi hivyo kuwa na upeo mpana wa mashirkiano hayo.
Mkurugenzi wa Soko la Ajira na Mipango na Maendeleo (VETA), Enock Kibendela, yeye alisema mafunzo haya yatasaidia kufungua soko la ajira kwa wahitimu na kusukuma mbele maendeleo ya nchi.
“Utekelezaji wa kuanzishwa kwa mafunzo haya kumekuja wakati muafaka kwani kufuatia agizo la serikali kuwa na vyuo vya ufundi katika kila wilaya kutakuwa namahitaji ya walimu katika sekta hii ya wakufunzi wa mafunzo ya elimu ya ufundi,” alifafanua.
Wanafunzi waliopata fursa ya kuzungumzia fursa hiyo mpya, walisema imekuja wakati mwafaka ambapo serikali inajizatiti kuhimiza uchumi wa viwanda unaohitaji wataalamu waliofundishwa elimu ya ufundi kwa viwango vya juu vyenye ushindani kimataifa.
Habari hii imeandaliwa na Vincent Mpepo na Ruth Kyelula wa OUT.
0 comments: