Advertisement |
Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia ulinzi wa amani, El Ghassim Wane, amesema changamoto
zinazoikabili Sudan Kusini zinatakiwa kuondolewa, ili kutumia fursa ya
uwepo wa vikosi vya ulinzi wa usalama kuirudisha nchi hiyo kwenye hali
ya utulivu na usalama.
Ameongeza kuwa kila juhudi inatakiwa kufanywa kuhakikisha kuwa "mjadala wa kitaifa" unakuwa shirikishi, wazi na unafanyika katika mazingira huru na salama na kuungwa mkono kwa maafikiano makubwa ya kisiasa.
Pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuifahamisha serikali ya Sudan Kusini kuwa hali ya sasa haikuibaliki na si ya kudumu.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Desemba 2013, vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Hivi sasa Machar yuko uhamishoni nchini Afrika Kusini huku nchi hiyo changa zaidi duniani ikiendelea kushuhudia mapigano baina ya vikosi vya serikali na waasi na hivyo kupelekea makumi ya maelfu ya watu kukimbilia usalama katika nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa za kupatanisha pande hasimu hadi sasa hazijazaa matunda.
0 comments: