Advertisement |
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, amevipongeza vyombo vya
habari nchini kwa mchango wake katika vita dhidi ya ujangili nchini.
Sambamba na pongezi hizo, ametoa
rai kwa vyombo hivyo kuongeza bidii katika kuelimisha jamii juu ya
umuhimu wa uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa kwa faida ya jamii
iliyopo na vizazi vijavyo.
Alitoa kauli hizo wakati akifungua mkutano wa
sita wa mwaka wa wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo vyote vya
habari nchini ulioandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) jijini Tanga huku kaulimbiu ya mkutano huo ikiwa UTALII WA
TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA.
"Ujangili
bado upo, Majangili tumepambana nao kweli kweli, na ninyi wanahabari
mmetusaidia sana katika kuhabarisha jamii juu ya matukio ya kukamatwa
kwao na hukumu wanazozipata, jambo ambalo limesaidia kujenga uoga kwa
watu kushiriki katika vitendo hivyo", alisema Maghembe.
Alisema
hofu hiyo pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na ujangili
imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujangili nchini hasa
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo mizoga ya tembo
inayotokana na ujangili imeonekana kupungua kwa kiasi kikubwa
ukilinganisha ni miaka iliyopita.
Akizungumzia
changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema sheria za
uhifadhi zinakataza watu kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa
kisheria, hivyo ni wajibu kwa wanahabari kuelimisha jamii juu ya umuhimu
wa kutii sheria hizo. "Ni vema wanahabari wakatumia kalamu zao vizuri
kuelimisha jamii juu ya athari za muingiliano wa binadamu, mifugo na
wanyamapori".
Alisema
wanyamapori wanabeba virusi vya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya
bonde la ufa, ndigana, kifua kikuu, homa za vipindi (brucolosis) na
kimeta, Magonjwa ambayo yanaweza pia kuambukiza mifugo na binaadamu
wanaoishi karibu na wanyamapori. Alisema kuwa endapo muingiliano huo
utaendelea kuwepo kwa muda mrefu unaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa
magonjwa hayo kwa binaadamu na mifugo hivyo kusababisha vifo vingi kwa
wakati mmoja.
Prof.
Maghembe alisema kumekuwepo na kisingizio cha kumega maeneo ya hifadhi
nchini kwa ajili ya matumizi ya kawaida kutokana na ongezeko la wananchi
jambo ambalo sio sahihi na kwamba njia pekee na salama ni kubadili
mfumo wa matumizi ya rasilimali zilizopo ikiwepo ya ardhi kwa kutumia
sayansi na teknolojia na kuweka matumizi bora ya ardhi kwa kulenga
matokeo chanya.
Akizungumzia
sekta ya utalii, Prof. Maghembe alisema wanahabari wanapaswa kuwa
sehemu ya kukuza uchumi wa nchi kwa kushiriki moja kwa moja katika
utoaji wa taarifa sahihi kwa Watanzania na wageni kuhusu sekta hiyo bila
ubaguzi wa aina yeyote.
"Tuipende
nchi yetu, tuitangaze na kuilinda, na katika habari hizi za uchumi
tuweke itikadi zetu pembeni tuandike habari za kujenga nchi yetu",
alisema Prof. Maghembe.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Alan Kijazi
amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na
asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema asilimia 80 ya
wageni wanaokuja nchini wanatembelea hifadhi za Taifa hususan za ukanda
wa Kaskazini jambo ambalo linaweka msukumo wa kuendeleza na kutangaza
hifadhi za nyanda zingine ili kuongeza idadi ya watalii na pato la
taifa.
Akizungumzia
mchango wa TANAPA katika uchumi wa taifa, Kijazi alisema mchango huo
umeongezeka ambapo katika mwaka 2015/2016 shirika hilo lilichangia
Shilingi bilioni 27 katika mfuko mkuu wa Serikali na mwaka 2016/2017
likachangia bilioni 34 sawa na ongezeko la bilioni saba.
Pamoja
na mafanikio hayo alisema jukumu la kuendeleza uhifadhi nchini haliwezi
kufanikiwa kwa jitihada za Serikali pekee bila kushirikisha wananchi
kupitia vyombo vya habari, Hivyo akatoa rai kwa wanahabari kuiunga mkono
Serikali katika kunadi sera za uhifdhi endelevu kwa maslahi ya taifa.
0 comments: