Sunday, July 30, 2017

Serikali yakana kupanga njama na jeshi

ad300
Advertisement
Waziri wa Ulinzi wa Kenya amekanusha madai ya kambi ya upinzani nchini humo kuhusiana na tuhuma za wizi wa kura na kukitetea Kikosi cha Ulinzi cha nchi hiyo (KDF), kuwa hakina mpango wowote wa kuiba kura kwa manufaa ya upande wowote.

Raychelle Omamo, akizungumza na wanahabari jijini Nairobi jana Julai 31, alisisitiza kuwa serikali haina mpango wa kuiba kura kama inavyozushwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani majukwaani.

"Hatuna mpango wowote wa kuiba kura kama inavyodaiwa. Maofisa wa jeshi wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na katiba.

"Katiba ya nchi imeweka wazi kuhusu kazi za maofisa wa KDF na uhalisia ni kwamba tunafanya kazi kwa kuzingatia sheria," alisema.

Matamshi hayo ya Waziri wa Ulinzi wa Kenya  yalitolewa kufuatia madai ya kiongozi wa muungano wa upinzani National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, aliyenukuliwa juma lililopita akisema maofisa wa KDF wanashirikiana na serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ili kumsaidia kutetea kiti chake kwa awamu ya pili na ya mwisho kwa kuiba kura.

Raila Odinga anayewania kiti cha Urais kwa tiketi ya Muungano wa NASA alinukuliwa Ijumaa akidai kuwa na taarifa juu ya maofisa wakuu wa KDF kufanya mkutano wa siri katika Ikulu ya Rais kupanga namna ya kuiba kura katika uchaguzi ujao wa Rais.

Inadaiwa kwamba kwenye tuhuma hizo, alionyesha orodha ya maofisa hao lakini Waziri Raychelle alikanusha kutambua orodha hiyo wala majina yaliyomo.

Naye Waziri wa Usalama wa Ndani Dk. Fred Matiang'i, alisema idara ya jeshi inafanya kazi ili kuimarisha usalama wa taifa na kuwataka wananchi kupuuza madai ya njama za wizi wa kura dhidi ya jeshi la KDF.

Uchaguzi mkuu wa Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Polisi nchini humo wamemuuwa kwa kumpiga risasi mshambuliaji ambaye aliingia kwa nguvu nyumbani kwa naibu wa rais nchini Kenya, Willliam Ruto.

Inaelezwa kuwa wakati wa tukio hilo, Ruto na familia yake hawakuwa ndani ya nyumba hiyo iliyoko katika kijiji kimoja karibu na mji wa Eldoret.

Taarifa ya Polisi inasema Mwanamume huyo aliingia nyumbani kwa naibu rais baada ya kumjeruhi mlinzi wa mlango kwa kitu chenye ncha kali kisha kumnyanganya bunduki yake.

Mkuu wa polisi, Joseph Boinet, aliviambia vyombo vya habari kuwa hali sasa imedhibitiwa kwa sababu uchunguzi umebaini alikuwa mshambuliaji pekee tofauti na ilivyoripotiwa awali kwamba lilikuwa kundi la watu.

Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: