Monday, July 17, 2017

CUF Magomeni kumng'ang'ania Kubenea

ad300
Advertisement
Chama cha Civic United Front (CUF) katika kata ya Makurumla, jijini Dar es Salam, kimetangaza vita dhidi ya mbunge wa jimbo la Ubungo, Saed Kubenea.

Vita hivyo vilivyotangazwa na chama hicho wilayani Ubungo, vimeelezwa kusababishwa na kitendo cha Kubenea kutangaza Operesheni Ondoa Msaliti Buguruni (OMB)
na kumuunga mkono Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad.


Mwenyekiti wa CUF Makurumla, Issa Njoka, alisema wanashangazwa na hatua ya Kubenea kuisemea CUF, wakati hana uhusiano na chama hicho.

Alisema watapambana na mbunge huyo kwa kila hatua, pindi atakapojaribu kwenda kwenye matawi ya CUF kama alivyokusudia kufanya.

“Tulisikia tamko la Kubenea kama Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki ya CHADEMA, wanataka kuvamia Buguruni, ikiwemo kuja kwenye baadhi ya matawi ya kata yetu ya Makurumla. Tunamkaribisha kwa mikono miwili na akijaribu kufanya hivyo, tutamuonyesha tafsiri sahihi ya ngangari,” alisema.

Aliongeza: “Kubena hana tena nasaba na CUF, anapatwa na nini kuisemea CUF? Ajue tulikutana kwenye UKAWA mwaka 2015 na baada ya uchaguzi kuisha, kila chama kimerudi kujenga harakati zake na kwa tafsiri nyepesi hapo ndipo UKAWA ilipoishia.”

Pamoja na hayo, alisema: “Kama anataka kuja CUF, anakaribishwa maana aliwahi kuwa msaidizi wa Mwenyekiti Profesa Lipumba na aliondoka mwenyewe, hivyo kama anataka kurudi CUF, tujue kama bado ni mwanachama, sio vinginevyo."

Aidha kiongozi huyo alisema wanaunga mkono hotuba ya Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya, kwa kutangaza mapambano ya jino kwa jino na CHADEMA, kwa madai kuwa, wamekuwa wakichochea mgogoro ndani ya chama hicho.

Alisema kwa sasa kumekuwa na hujuma za wazi ndani ya CUF, ikiwemo watu wa nje kuchochea mgogoro huo ili kutafuta huruma ya kuonekana ni nani anayefaa kupendwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif.

“Wapo wanachama na viongozi, ambao sasa kazi yao ni matusi dhidi ya Profesa Lipumba. Tunawaambia vitendo vyao hivyo chini ya uratibu wa CHADEMA, katu haviwezi kumuondoa mwenyekiti wetu, warudi tujenge chama pamoja, badala ya kuendeleza matusi ambayo si misingi ya kuanzishwa kwa CUF,” alisisitiza.

Wiki iliyopita, Kubenea alitangaza msimamo wa kumuunga mkono Maalim Seif kwa kutangaza Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni, kwa lengo la kuisaidia CUF.

Mbali na hilo, alitangaza kutembelea matawi ya Ukanda wa Gaza, Mashujaa la Mwembe Chai, Chechinia na Kosovo ili kuuhisha matawi hayo na kurudisha hamasa ya CUF.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: