Monday, September 12, 2016

Simba yafanya kweli uwanja wa Uhuru, Dar

ad300
Advertisement
Mshambuliaji wa Simba, Leudedit Mavugo
Timu ya Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’, imezidi kuchanja mbuga katika mbio za kuwania ubingwa, baada ya jana kuigagadua Mtibwa Sugar mabao 2-0.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwa kiasi fulani mchezo huo ulipoteza ladha kutokana na baadhi ya sehemu ya uwanja kujaa maji.

Dar es Salaam jana mvua ilianza kunyesha mchana katika maeneo mbalimbali ya Jiji.
Timu hizo zilianza mchezo kwa kasi na dakika ya tano Simba ilibisha hodi langoni mwa Mtibwa Sugar, lakini ilishindwa kufunga bao kupitia kwa Laudit Mavugo.

Mpira ulichezwa katikati ya uwanja huku wachezaji wakicheza kwa tahadhari kuogopa utelezi.
Simba ilifanya shambulizi dakika ya 24, lakini shuti la straika, Ibrahim Ajib lilidakwa na kipa wa Mtibwa, Abdallah Makangana.

Mtibwa iliipenya ngome ya Simba dakika ya 34 na mshambuliaji, Haruna Chanongo alikosa bao, baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Vincent Angban.

Chanongo, alikuwa mchezaji wa Simba kabla ya kupelekwa kwa mkopo Stand United na msimu huu ameibukia Mtibwa.

Dakika ya 50 Mtibwa ilifanya shambulizi la kushitukiza langoni mwa Simba na beki Kelvin Idd, alishindwa kufunga mbele ya Angban.

Simba ilijibu shambulio hilo kwa kupata bao la kwanza dakika ya 53 likiwekwa wavuni na Ibrahim Ajib.

Ajib, alifunga bao hilo baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na winga machachari, Shiza Kichuya.

Simba ilizidisha mashambulizi langoni mwa Mtibwa na kupata bao la pili dakika ya 66 lililofungwa na mchezaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo.

Beki wa kushoto wa Mtibwa, Issa Rashid, aliitoka ngome ya Simba, lakini shuti lake lilitoka nje dakika ya 72.

Simba: Vincent Angban, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Shiza Kichuya.Frederick Blagnon, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib na Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla.

Mtibwa: Abdallah Makangana, Ali Sharifu, Issa Rashid, Kassim Ponera, Salim Abdallah, Kelvin Idd, Ali Yussuf, Stamili Mbonde/Said Mkopi, Ibrahim Juma na Haruna Chanongo.
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 comments: