Advertisement |
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeanza
kutekeleza programu endelevu za kutoa elimu ya mpiga kura ili kuwaelimisha
wananchi waliofikisha umri wa kupiga kura kutekeleza wajibu na haki yao
kikatiba kwenye upigaji wa kura katika chaguzi zijazo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani, wakati akizungumza na waandishi wa
Habari mjini Musoma kuhusu mkakati wa NEC wa kuwafikia wananchi moja kwa moja
kuwapatia elimu ya mpiga kura.
Alisema kuwa Tume hiyo imeanza kutoa elimu
hiyo kwa kushiriki maonesho na mikutano mbalimbali ukiwemo mkutano wa Jumuiya
ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika mjini Musoma kuanzia
Septemba 22 hadi 24, mwaka huu.
“Tumeamua kushiriki kwenye mkutano huu kwa
kuwa hawa ni watendaji wa Serikali katika ngazi za mitaa, tumekuja kutoa elimu
ya mpigakura kwani suala la elimu tunalipa kipaumbele” alisema Kailima.
Aidha alisema Tume imeandaa programu
ya kuwafikia wapiga kura moja kwa moja kwa kuweka mkakati wa kuhudhuria
mikutano yote ambayo iko kihalali ikijumuisha ile ya Mawaziri na Naibu Mawaziri
, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
Alibainisha kuwa tayari NEC imewasiliana na
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili iweze kupata
ratiba ya vikao vya kamati za ushauri za mikoa na wilaya ili iweze kupata fursa
ya kutoa elimu ya mpiga kura ndani ya vikao hivyo.
Kailima alifafanua kuwa Tume imemwomba
Katibu Mkuu TAMISEMI, ratiba ya vikao vya Mabaraza ya madiwani ya halmashauri
zote nchini kwa lengo la kuwezesha wataalamu wa Tume hiyo kutoa elimu ya Mpiga
kura.
“Tumemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI atusaidie
kuweka ajenda ya kudumu kuhusu utaratibu mzima wa uendeshaji wa uchaguzi na
uelimishaji wa mpiga kura kwenye vikao vya mabaraza ya Madiwani ambapo maafisa
wa Tume walio katika ngazi za halmashauri watapata fursa ya kutoa elimu ya
mpiga kura katika vikao hivyo” alisema.
Aliendelea kusema kuwa NEC imejipanga
kupanua wigo wa utoaji wa habari kupitia vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii ili kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu ya mpiga kura
na taarifa sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na majukumu yake.
“Tumejipanga kutumia vyombo vya habari,
kila wiki tutakuwa na taarifa na mada fupifupi zinazohusu mchakato mzima wa
uchaguzi kwa maana ya uandikishaji na zoezi zima la upigaji kura kujenga uelewa
kwa jamii nzima kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
Aidha alisema kuwa kifungu Na 4 (c) cha
Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kinaelezea wazi kuwa pamoja na mambo mengine
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu kutoa elimu ya Mpiga kura, kuratibu
Taasisi na watu wenye uwezo wa kutoa elimu ya mpiga kura ili kuongeza
uelewa miongoni mwa jamii.
“Tunategemea kuanzia mwanzoni mwa mwezi
Oktoba tutatoa tangazo la kuzialika Asasi na taasisi zinazotaka kutoa elimu ya
mpiga kura ziwasilishe maombi yao Tume ya Uchaguzi pamoja na zana zao za
kutolea elimu ili tuweze kuwapatia kibali cha miezi 6 na baadaye tutafanya
tathmini juu ya ufanisi wa kazi wanayoifanya,” alisema Kailima.
Alisema lengo la kuzishirikisha taasisi na
Asasi hizo ni kuondoa ombwe lililokuwa linaonekana la utoaji wa elimu ya mpiga
kura wakati wa uchaguzi pekee kwa kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kila wakati
ili kuongeza uelewa wa wananchi katika chaguzi zijazo.
Aidha, alisema NEC imeandaa mpango mpya wa
kuzifikia shule mbalimbali za Sekondari hapa nchini utakaowawezesha wanafunzi
wa shule zitakazochaguliwa kuwa na Klabu za elimu ya mpiga kura.
Alisema programu hiyo itaiwezesha Tume
kuwaelimisha wanafunzi waliofikisha umri wa kupiga kura na wale ambao bado
hawajafikia umri huo ili kujenga uelewa wao kuhusu elimu ya Mpiga kura.
“Tumeanza program hii kwa kuzitembelea
shule mbili za Sekondari za Isange (wasichana) na Shule ya Ufundi Musoma zilizo
katika Manispaa ya Musoma, tutaongea na wanafunzi waliofikia umri wa kupiga
kura lakini bado hawajajiandikisha kupiga kura na wale ambao bado hawajafikisha
umri wa kupiga kura, tumenalenga kuanzisha klabu ya Elimu ya mpiga kura kwenye
shule moja katika kila wilaya ya Tanzania,” alisema.
Kuanzishwa kwa klabu hizo kutawawezesha
wanafunzi kujadiliana kwa kina kuhusu mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura kwa
mujibu wa sheria iliyopo ili kufikia lengo la kuwa na shule moja yenye Klabu ya
elimu ya mpiga kura katika kila wilaya ifikapo Januari 2020.
0 comments: