Advertisement |
Mahakama ya wilaya Tarime mkoani
Mara, imemhukumu Mashaka Marwa kifungo cha miaka 30 jela, kwa kosa la kumbaka
mwanafunzi wa darasa la sita.
Pia imemhukumu amlipe mlalamikaji
faini ya sh. milioni 4 akitoka gerezani na kuchapwa viboko sita kwa kosa hilo
ambalo lilimfanya amuambukize mwanafunzi huyo wa shule ya msingi Sabasaba
ugonjwa wa kisonono.
Akisoma shitaka hilo mbele ya
hakimu Amon Kahimba, Mwendesha mashitaka wa Polisi, Mwanri Mrisho, alidai Machi
12, mwaka huu, saa 9 mchana, mlalamikaji alitoka na kwenda kwenye shamba la
Babu yake kujisaidia baada ya choo chao kubomoka.
Alidai baada ya kuvua nguo
alivamiwa na kukabwa nyingoni na mtuhumiwa huku akimtishia kumuua kwa kumchoma
kisu endapo angepiga kelele, kisha kumpiga ngwala na kuanza kumbaka.
Mwanri alidai mtoto huyo alipiga
kelele za kuomba msaada kutokana na maumivu aliyoyapata lakini hakukuwa na mtu
maeneo ya karibu hivyo mtuhumiwa alimaliza haja yake na kutoroka.
Mwendesha mashitaka huyo
aliendelea kueleza kuwa baada ya kitendo hicho, mtoto huyo wa miaka 13 alirudi
nyumbani kwa Babu yake (Siongo Marwa) na kumweleza yaliyompata ambapo walirudi
mpaka eneo lile na kuona mahindi yamevunjwa kutokana na purukushani.
Alidai Mzee Siongo (Babu wa
mtoto), alimchukua mjukuu wake mpaka kituo cha polisi ambapo walipewa PF3 na
kwenda hospitali walikofanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kuthibitishwa kuwa
amebakwa na kuambukizwa ugonjwa wa kisonono.
Mwanri aliiomba mahakama kumpa
mtuhumiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo, kwa sababu
imemuharibia Mwanafunzi huyo usichana wake na kumwambukiza ugonjwa wa zinaa.
Baada ya maelezo hayo, Mtuhumiwa
alijitetea na kudai kuwa ameshitakiwa kutokana na mgogoro wa ardhi na viwanja
kati ya Babu wa Mwanafunzi huyo na Mama yake mzazi hivyo kuiomba Mahakama
kumsamehe huku akiomba nakala ya hukumu
kwa ajili ya Rufaa.
Akitoa maamuzi ya kesi hiyo,
Hakimu wa Mahakama hiyo, Amon Kahimba, alidai ameridhika na ushahidi uliotolewa
na upande wa mlalamikaji mahakamani hapo bila shaka yoyote huku upande wa
mshtakiwa ukikosa shahidi.
Alidai hawezi kumpa nakala ya
hukumu kutokana na kwamba hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa kuna migogoro ya
ardhi baina ya wazazi ambapo hata mzazi wake, hakufika kutoa ushahidi.
Hakimu huyo alidai kwa viashiria
hivyo inaonyesha huenda mtuhumiwa alitaka kujiokoa kwa kutumia kisingizio cha
migogoro ya ardhi hivyo anastahili kuhumu kwa mujibu wa sheria.
Upande wa Mlalamikaji ulikuwa na
mashahidi 6 akiwemo mwanafunzi huyo, Babu yake aliyeambatanisha fomu ya majibu
ya vipimo hospitalini, tabibu aliyemhudumia mlalamikaji na mpelelezaji wa kesi
hiyo.
0 comments: