Advertisement |
Mikoa
ya Dar es Salaam na Pwani, hususan maeneo yanayopata huduma ya maji safi kutoka
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), yatakosa huduma hiyo
kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Chini.
Akizungumza
na Uhuru jana jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa shirika hilo,
Everlasting Lyaro, alisema mitambo hiyo iliyoko mkoani Pwani itazimwa kwa
wastani wa saa 12 kesho (24/09/2016), kwa ajili ya matengenezo kwenye njia ya umeme.
Everlasting
alisema wamelazimika kuizima mitambo
hiyo ili kuruhusu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufanya matengenezo
kwenye laini kubwa ya umeme inayotoka Ubungo kwenda kituo cha chake cha Mlandizi.
Alisema
kituo hicho cha umeme kilichoko Mlandizi mkoani Pwani, ndicho kinachotegemewa kunapeleka
umeme kwenye mitambo ya maji ya Ruvu juu na Ruvu chini.
“Kutokana
na Matengenezo hayo yatakayofanywa na TANESCO kutakuwepo na ukosefu wa huduma
ya maji kwa wakazi wa Mlandizi mjini, Ruvu darajani, Vikuruti, Disunyara,
Kilangalanga, Janga, Mbagala, na Visiga, mkoani Pwani,” alisema.
Maeneo
mengine aliyataja kuwa ni Maili 35, Zogowale, Misugusugu, Tanita, Kibondeni,
Kwa Mathias, Nyumbu, Msangani, Kwa Mbonde, Picha ya Ndege, Sofu, Lulanzi,
Gogoni, Kibamba, Kibamba Njia Panda, Shule Kibwegere, Mloganzira, Kwembe, Kibamba
Hospitali, Kwa Mkinga na Luguruni.
Aidha
aliyataja maeneo mengine yatakayoathiriwa na kuzimwa kwa mitambo ya Ruvu juu na
chini kuwa ni Mji wa Bagamoyo, vijiji vya Mapinga, Kerege na Mapunga pia Bunju,
Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Jangwani, Mbezi Beach na Kawe.
“Mlalakuwa,
Mwenge, Mikocheni, Msasani, Sinza, Manzese, Mabibo, Kijitonyama, Kinondoni,
Oysterbay, Magomeni, Upanga, Kariakoo, City Centre, Ilala, Ubungo Maziwa,
Kigogo, Mburahati, Hospitali Ya Rufaa Muhimbili, Buguruni, Changombe, Keko pamoja
na Tabata pia kutaarithiwa na matengenezo haya,” alisema.
Kutokana
na hatua hiyo, Meneja huyo alisema DAWASCO inawaomba radhi wananchi na kwamba
wanapaswa kuhifadhi maji kwa kipindi hiki, ili wasipate shida wakati mitambo
hiyo itakapozimwa.
0 comments: