Advertisement |
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limeanzisha
utaratibu wa kukutana na wateja wake kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri baina
ya shirika na wateja hao.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Usambazaji Huduma
kwa Wateja wa TANESCO, Sophia Mjema, alisema utaratibu huo utaboresha uhusiano
baina ya shirika na wateja pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto
zinazojitokeza.
Alisema wameanza kukutana na wateja wakubwa na baadae
watakutana na wateja wa kati na wadogo ili kuongeza ufanisi na utendaji.
Sophia alisema hivi sasa shirika linahakikisha umeme
unazalishwa kwa wingi na unawafikia wateja kwa wakati na kwamba lengo la
TANESCO ni kwenda kibiashara zaidi.
Akizungumza kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika
hilo kwa kampuni ya Helios Towers inayosambaza umeme kwenye minara ya simu
nchini, Sophia alisema shirika litaendelea kuboresha huduma zake ili ziende na
wakati.
Sophia alisema wateja wakubwa kama kampuni za simu
zimefungwa mita maalumu ambazo zinasomeka moja kwa moja kwenye ofisi za TANESCO
na kwamba mfumo huo umesaidia kudhibiti wizi wa umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Helios
Towers, Alexander High, alisema kampuni hiyo inauza umeme kwenye minara ya
kampuni za simu nchini.
Alisema umeme huo wananunua kutoka TANESCO na kuuza
kwenye kampuni hizo ambapo asilimia 70 ya minara inatumia umeme na asilimia 30
inatumia jenereta.
0 comments: