Advertisement |
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba |
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba alisema Israel tayari imewaua Wapalestina wapatao 296 wengi wao wakiwa ni raia wasio na hatia.
Alisema raia hao wako watoto na wanawake huku kukiwa na majeruhi maelfu kwa maelfu tangu mashambulizi hayo yalipoanzishwa Julai 8 mwaka huu.
Aidha alisema mashambulizi hayo yanayodaiwa kufanywa ili kukabiliana na chama cha Hamas kinachoongoza Gaza baada ya kuchaguliwa na wananchi wa eneo hilo kwa njia za kidemokrasia, yanaonesha kiasi gani Israel haiheshimu utu na misingi ya haki za binadamu.
"Mashambulizi haya hayasaidii chochote katika kutafuta suluhisho la kudumu na la maana la mgogoro wa Mashariki ya Kati. Yanaonesha dhahiri jinsi Israel walivyo wanyama na haki za binadamu. Zaidi ya yote yanaongeza chuki za Wapalestina dhidi ya Israel na jumuiya ya kimataifa wanayoiona haichukui hatua zozote dhidi ya unyama wanaofanyiwa," alisema Lipumba.
Hata hivyo alisema Israel haipaswi kujificha nyuma ya kivuli cha mashambulizi ya Hamas huku yenyewe ikiwa inaendelea kuvunja Maazimio 65 ya Umoja wa Mataifa dhidi yake yaliyopitishwa baina ya 1955 – 1992 na mengine kadhaa yaliyopitishwa baada ya hapo.
Mwenyekiti huyo alisema wanaishurutisha serikali ifanye kitu katika kuheshimu misingi ya Chama chao ambacho kimejikita katika kutambua na kuenzi haki za binadamu na haki za watu sambamba na kwa kutambua msimamo thabiti wa Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere wa kusimama pamoja na Wapalestina katika kupigania haki zao.
Lipumba alisema moja ya wajibu wa Serikali ya Tanzania ni kutoa tamko la kulaani mashambulizi hayo na kuitaka Israel iheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa na haki ya kuwepo kwa Taifa huru la Palestina.
0 comments: